Serekali ya Misri imesema kwamba itaendelea na juhudi zake leo za kuiondoa meli kubwa ya makasha iliyokwama na kuziba mfereji wa Suez.
Oparesheni hiyo itafanywa kwa msaada wa boti zenye nguvu, ili kufungua njia hiyo muhimu kwa biashara ya usafirishaji shehena kwa njia ya bahari iliyozibwa kwa takriban wiki moja sasa.
Mfereji huo ambao unaunganisha bahari ya Sham na Mediterranean unatarajiwa kuongezeka kwa kina cha maji leo hii.
Wachimba mchanga kuongeza kina cha mfereji waliendelea na kazi usiku kucha wakijaribu kuondoa kingo za mfereji ili kusaidia meli hiyo kubwa kuelea na kuondoka katika eneo hilo.
Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa kuna uwezekano wa kuwepo kwa jiwe kubwa chini ya mahala ambapo meli hiyo imekwama.
Mpaka sasa kiwango kikubwa cha mchanga kimesha ondolewa kuzunguka meli ya Ever Given iliyokwama.