Jeshi laweka sheria kali zaidi Myanmar

Waandamanaji wa Myanmar katika maandamano ya kupinga mapinduzi ya kijeshi.

Serekali ya kijeshi ya Myanmar imeongeza muda wa sheria za kijeshi katika maeneo zaidi ya mji mkuu Yangon, Jumatatu huku kukiwa na ripoti kwamba wandamanaji zaidi wameuwawa na vikosi vya usalama.

Kundi la utetezi la wa wafungwa wa kisiasa (AAPP), ambalo limekuwa likifuatilia ghasia za nchini humo, limesema kwamba takriban watu 20 waliuwawa Jumatatu katika mashambulizi ya risasi.

Televisheni ya serekali ya MRTV imetangaza kwamba wilaya za North Dragon, South Dragon, Dagon Seikkan, na North Okkalapa ziko chini ya sheria za kijeshi kutokana na maandamano ya mwishoni mwa juma ambayo yalikuwa mabaya.

Katibu mkuu wa umoja wa mataifa, Antonio Guterres amesema Jumatatu kwamba anasikitishwa na kuongezeka kwa ghasia nchini Myanmar na zinazofanywa na jeshi la nchi hiyo, kwa mujibu wa msemaji wake.