Rais wa marekani Joe Biden Alhamisi, alitia Saini muswada wa afueni kwa corona wa dola trillioni 1.9 na hivyo kufungua njia ya kutoa msaada wa fedha wa serekali kuu kwa wamarekani na wafanyabiashara wanaotaabika kutokana na janga la Covid.
Biden ambae ni mdemocrat, amesaini muswada huo siku moja baada ya baraza la wawakilishi kuupitisha kwa kura 220 dhidi ya 211 bila uungwaji mkono wa wabunge wa chama cha republican.
Amesaini pia mswaada huo siku moja kabla kama ilivyokua imetangazwa na White House kwamba atausaini Ijumaa hii.
“Sheria hii ya kihistoria ni kwa ajili kujenga nguvu ya kiuchumi katika nchi hii na kuwapa watu katika nchini, wafanyakazi, watu wa tabaka la kati, watu waliojenga nchi hii, nafasi ya kupambana”, Biden amesema wakati akijiandaa kusaini muswada huo.
Wabunge wa republican wameupinga mswaada huo wakisema umetenga pesa nyingi sana na haukulenga vya kutosha wale wanaohitaji msaada wa kiuchumi.
Sheria hiyo mpya inatoa dola elfu 1 na 400 kwa watu wazima wenye pato la chini ya dola elfu 80 kwa mwaka, umepunguzia mzigo wa kodi pia familia zenye pato la chini kwa kutoa dola elfu 3 kwa mtoto alie na umri wa miaka 6 hadi 17, na dola elfu 3 na 600 kwa Watoto walio chini ya miaka 6 katika mwaka wa kodi wa 2021.
Nao wafanyakazi waliopoteza ajira wataendelea kupokea mafao ya dola 300 kwa wiki hadi mapema mwezi Septemba mwaka huu.
Serekali za majimbo na wilaya zitapewa dola billioni 350 ili zijikwamuwe kiuchumi baada ya kukumbwa na janga la corona.