Wabunge Marekani watenga pesa kwa ajili ya kusaidia biashara na watu wasiokuwa na ajira

Wabunge nchini Marekani wamekubaliana kuhusu pesa za kusaidia biashara na watu wasiokuwa na ajira, kiasi cha dola bilioni 900, baada ya malumbano ya miezi kadhaa.

Pesa hizo zinatarajiwa kuwa sehemu ya dola trilioni 1.4 zitakazotumika kugharamia shughuli za serikali kwa mda wa miezi tisa ijayo.

Makubaliano hayo yamefanyika siku chache kabla ya siku ya mwisho ya kumalizika kwa ufadhili wa mipango ya kupambana na janga la virusi vya Corona hapa Marekani.

Karibu wamarekani million 12 walikuwa katika hatari ya kukosa kupata pesa zinazotengewa watu wasiokuwa na ajira.

Baraza la wawakilishi Pamoja na senate, wanatarajiwa kupiga kura kuhusu makubaliano hayo, baadaye leo jumatatu.

Mswada huo utahitaji kusainiwa na rais Donald Trump kabla ya kuanza kutekelezwa.

Idadi kubwa ya raia wa Marekani watapewa dola 600 kuwasaidia kujikimu kimaisha huku dola 300 zikiwa zimetengewa watu wasiokuwa na ajira, kila wiki.

Zaidi ya dola bilioni 300 zitatumika kusaidia wafanyabiashara na kusambaza chanjo dhidi ya virusi vya Corona.