Miaka 3 ya Mnangagwa Zimbabwe yaghubikwa na visa vya kubana uhuru wa kujieleza

Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa

Imetimia miaka 3 tangu rais Emmerson Mnangagwa alipoingia madarakani kutoka kwa marehemu Robert Mugabe na kuahidi kuheshimu haki za binadamu kwa mujibu wa katiba.

Lakini wakosoaji wake wanasema kwamba uhuru wa habari nchini Zimbabwe hauheshimiwi, wakitoa mifano ya kukamatwa kwa waandishi wa habari maarufu mwaka huu.

Hopewell Chinono ni mwandishi wa habari nchini Zimbabwe. Amekamatwa mara mbili mwaka huu baada ya kuandika ujumbe wa twitter.

Katika ujumbe wa kwanza alioandika mwezi July, Chinono aliunga mkono maandamano ya kupinga ufisadi serikalini.

Ujumbe wa pili wa mwezi Novemba ambapo alimkosoa jaji mkuu wa Zimbabwe.

Amefunguliwa mashtaka ya kuchochea ghasia na kuzuia haki kutendeka Pamoja na kudharau mamlaka ya kitaifa ya waendesha mashtaka.

Chin’ono anasema kwamba mamlaka inatuma ujumbe wa wazi kutokana na kukamatwa kwake, na kwamba waandishi wa habari nchini Zimbabwe wanasikiliza.

“Kwa sababu ya kukamatwa, waandishi wameingiwa na uoga na kufanya yaliyo ya haki katika kufanya kazi yao kwa sababu wanaogopa kukamatwa. Wana hofu kwamba kwa sababu Chinono alikamatwa n ani mtu maarufu, basi wao wakikamatwa watafia gerezani.”

Rais wa zamani Robert Mugabe mara kwa mara alikuwa akitumia sheria zinazobana vyombo vya habari wakati wa utawala wake wa miaka 37.

Rais Munangagwa alipoingia madarakani mwaka 2017, aliahidi kuwepo uhuru wa kujieleza. Alitoa ujumbe wa matumaini kati ya waandishi wa habari na raia kwa jumla.

Maafisa serikalini wafutilia mbali shutuma za kubana uhuru wa habari

Maafisa serikalini wanasisitiza kwamba kukamatwa kwa Chinono ni hatua inayoambatana na kuheshimu sheria na wala sio ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari.

Ndavaningi Mangwana ni katibu katika wizara ya habari ya Zimbabwe.

“Hakuna mtu amekamatwa chini ya sheria yoyote inayohusiana na uhuru wa vyombo vya habari. Lakini kama sheria imevunjwa katika idhara nyingine ya usalama wetu, basi haijalishi kama ni mwandishi wa habari, wakili, daktari. Watu watakamatwa. Kando na hayo mazingira ya waandishi wa habari ni mazuri.”

Afisa huyo katika wizara ya habari amesema kwamba vituo sita vya televisheni vimepewa leseni hivi karibuni nchini Zimbabwe, na kwamba vituo vya habari vya kimataifa sasa vina uhuru wa kufanya kazi nchini humo.

Mswada wa kuzima habari kwenye mitandao ya kijamii

Lakini makundi ya kutetea uhuru wa habari yanasema kwamba serikali ya Zimbabwe haijaacha kukandamiza uhuru wa habari.

Tabani Moyo, ni mkuu wa chuo cha habari cha Media Institute of Southern Africa, nchini Zimbabwe:

“Tunapiga hatua moja mbele, halafu kumi nyuma. Msako dhidi ya waandishi wa habari za upekuzi unaendelea. Mfano ni dhidi ya Hopewell Chinono. Mashambulizi dhidi ya vyombo vya habari yamekuwa yakiongezeka. Sheria zinaendelea kutungwa kubana uhuru wa habari, mfano ni mswada wa usalama wa mitandao ambao lengo lake ni kutoa mamlaka kwa wanajeshi kukabiliana na watu wanaojieleza.”

Iwapo mswada huo wa kudhibithi mawasiliano kupitia internet utapitishwa na kuwa sheria, raia wa Zimbabwe watakaoshutumiwa kwa kueneza habari za uongo kupitia mitandao ya kijamii wanaweza kupata adhabu ya mahakama ya hadi kufungo cha miaka mitano jela.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC