Mwenyekiti wa chama kikuu upinzani tanzania, CHADEMA - Freeman Mbowe pamoja na wanachama zaidi ya 20 wa chama hicho wamekamatwa na polisi saa chache baada ya rais wa Tanzania John Magufuli, kuahidi kushirikiana na wapinzani wake, baada ya kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa wiki iliyopita.
Kwa mujibu wa kamanda wa polisi wa jiji la Dar es salaam, Lazarus Mambosasa, polisi imewakamata viongozi hao wa Chadema ili kuchukua hatua za tahadhari kusitokee vurugu ambazo zitaharibu amani. Wanachama wengine takriban 20 wamekamatwa mkoani Singida na kuna ripoti za wengine zaidi kukamatwa katika mikoa mbali mbali.
Wanasiasa wa upinzani ikiwa ni pamoja na mgombea urais wa chadema, Tundu Lissu, Mbowe na kiongozi wa chama kingine cha upinzania ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, Jumamosi waliitisha maandamano ya amani kupinga matokeo hayo ya uchaguzi kuanzia Jumatatu.
Akizungumza mjini Dodoma Jumapili mbele ya viongozi wa serikali cha chama cha CCM Rais Magufuli aliahidi kushirikiana na viongozi wote ikiwa ni pamoja na wa upinzani katika kuongoza nchi hiyo baada ya ushindi wake wa asilimia 84 katika uchaguzi wa wiki iliyopita.
“Nitawatumikia watanzania wote. Napenda kuwashukuru washindani wangu kwa kushiriki katika uchaguzi,” amesema Magufuli katika hafla ya kukubali rasmi ushindi wake mjini Dodoma.
Kulingana na matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi (NEC), Magufuli alipata asilimia 84 ya kura zilizopigwa, akifuatiwa na Tundu Lissu, aliyepata asilimia 13.
“Naahidi kushirikiana na nyinyi kuhakikisha kwamba tunapata maendeleo ya taifa. Maendeleo bila ubaguzi. Siasa sio vita, siasa sio fujo, sote ni watanzania.”
Jumamosi, chama cha Tundu Lissu cha CHADEMA, pamoja na chama cha upinzani cha ACT Wazalendo, vilikataa kutambua matokeo ya uchaguzi huo na kuitisha maandamano kote nchini Tanzania, kutaka uchaguzi mpya kuandaliwa.
Madai ya wizi wa kura yamegubika uchaguzi wa Tanzania, polisi wakishutumiwa kutumia nguvu dhidi ya raia, karatasi bandia za kura, wanasiasa wa upinzani kukamatwa na polisi na kuzuiliwa na mawakala wa vyama vya upinzani kuzuiwa kufuatilia uchaguzi huo. Madai haya yameorodheshwa pia katika taarifa ya ubalozi wa Marekani nchini Tanzania.
Uingereza pia imeyataja madai hayo katika taarifa yake na kutaka uchunguzi kufanyika. Waziri wa Maswala ya Afrika nchini Uingereza James Duddridge amesema kwamba Uingereza “imesikitishwa sana na ripoti za kutokea vurugu na polisi kutumia nguvu wakati wa uchaguzi pamoja na kuwakamata wanasiasa wa upinzani.”
Ritpoti ya waziri huyo imesema kwamba “hali ya utulivu na maendeleo nchini Tanzania inahitaji uchaguzi ulio huru na haki.”
Magufuli amesifiwa kwa kuanzisha miradi mikubwa ya maendeleo pamoja na kupambana na ufisadi.
Wakosoaji wake wamemshutumu kwa utawala wa kimabavu na kukandamiza wakosoaji, vyombo vya habari na kuzuia mikutano ya wanasiasa wa upinzani. Maafisa wa serikali ya Tanzania wamekuwa wakikanusha madai ya kuwepo utawala wa kimabavu nchini humo.
Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC.