Msuluhishi wa Umoja wa Mataifa katika mgogoro wa Libya anasema hatua ya kuridhisha imefikiwa baada ya siku mbili za mazungumzo ya ana kwa ana kati ya viongozi wa kijeshi wa pande zinagombana nchini Libya. Awamu ya nne ya mkutano wa kamati ya mseto ya kijeshi ambao una lengo la kufikia sitisho la kudumu la mapigano, inafanyika wiki hii mjini Geneva.
Kiongozi wa tume ya Umoja wa Mataifa nchini Libya Stephanie Williams, anasema pande hizo mbili zimefikia makubaliano kuhusu masuala kadha nyeti ambayo yataboresha moja kwa moja maisha na ustawi wa wananchi wa Libya.
Williams anasema wajumbe wanaoshiriki kwenye mazungumzo hayo wamekubaliana kufungua barabara zinazounganisha majimbo na miji yote ya Libya na kuruhusu safari za ndege zifanyike tena nchini kote.
Ameongeza kuwa pande zote zimekubaliana kuachana na kauli za uchochezi na kuwawajibisha wale wote wanaotumia matamshi ya chuki kwenye mitandao ya kijamii ili kuchochea ghasia.
Anasema viongozi wa kijeshi wamekubaliana pia kuunga mkono hali ya utulivu inayojiri wakati huu nchini kote na kuzuia mashambulizi ya kijeshi yasitokee tena. Williams anasema ana Imani kwamba makubaliano hayo yataheshimishwa kwa sababu ni suluhu iliyotafutwa na wa Libya wenyewe.
“Nadhani ninaiona hatua nzuri ambayo inaleta matumaini. Baada ya yote, ni nchi yao na Libya ni ya wa Libya wote. Ndio maana naendelea kuwa na matumaini kwamba pande hizo zitafikia makubaliano ya sitisho la mapigano la kudumu,” alisema.
Libya imekumbwa na mgogoro wa kivita tangu auwawe kiongozi wake wa zamani Moammar Gadhafi mwaka wa 2011.
Mvutano mkali wa kupigania udhibiti wa madaraka umekua ukiendelea kati ya serekali mbili hasimu, ile inayotambuliwa kimataifa yenye makao yake mjini Tripoli, na ile inayoongozwa na kamanda aliyeasi Jenerali Khalifa Haftar, ambayo ina makao yake mjini Benghazi.
Mapigano yamesitishwa miezi ya karibuni kutokana na shinikizo la jumuia ya kimataifa.
Pamoja na kuwa na matumaini kuhusu mazungumzo hayo, Williams anaona matatizo mengi ambayo yatajitokeza wakati pande mbili zitaanza kujadili kwa kina masuala magumu katika makubaliano.
“Ni kama tunakimbizana na muda kwa sababu ya hali inayojiri nchini, kusema ukweli kwa sababu ya kiwango cha uingiliaji mkali wa kigeni na ukiukwaji wa wazi wa vikwazo vya silaha.”
Uturuki inaiunga mkono serikali inayotambulika kimataifa ya mjini Tripoli, Russia na umoja wa Falme za Kiarabu ni miongoni mwa nchi washirika wa jeshi la Jenerali Haftar.
Nchi zote hizo zimekosolewa kwa kukiuka vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa na kuchochea vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoiharibu Libya.