Uwamuzi wa Marekani kubadili msimamo wake umekosolewa na Jumuia ya kimataifa siku ya Jumatatu, abapo mataifa mengi yamelaani uwamuzi huo.
Wapalestina wamakasirishwa na kulalamika dhidi ya uwamuzi wa Marekani kutambua makazi ya walowezi ya wayahudi kuwa ni halali baada ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Mike Pompeo kutangaza, Jumatatukwamba Washington inabadili msimamo wake kuhusiana na suala hilo.
Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya na Umoja wa Nchi za Kiarabu zimetoa taarifa kupinga uwamuzi huo na kukumbusha kwamba makazi yote ya wayahudi katika ardhi za wapalestina zinazokaliwa pamoja na Jerusalem Mashariki ni kinyume cha sheria za kimataifa na kutoa wito kwa Israel kusitisha kabisa upanuzi wa makazi ya walowezi.
Hadi hapo jana sera rasmi ya Marekani kwa misingi ya kisheria iliyotolewa na wizara ya mambo ya kigeni 1978, ilikua ni kwamba makazi ya walowezi kwenye ardhi za wapalestina yalikua yana kwenda kinyume na sheria za kimataifa.
Mgombea kiti cha rais wa chama cha Demokratic hapa Marekani Bernie Sanders katika ujumbe wa tweeter amesema, kuwepo na makazi ya walowezi wa kiyahudi kwenye ardhi zinazokaliwa za wapalestina ni kinyume cha sheria za kimataifa na kwamba rais wa Marekani ana hujumu juhudi za kidiplomasia.