Wanadai kuwa hata kuondoka mamlakani kwa Hailemariam Desalegn sio kwamba itakuwa jambo rahisi kuchochea mabadiliko ya msingi ya kisiasa.
Mapema wiki hii akizungumza na taifa, Desalegn alisema kuwa anaachia madaraka na kukaa kando ili kuisaidia nchi kufanya mageuzi ambayo yatapelekea amani na uthabiti nchini.
Nchi hiyo imeshuhudia wimbi la maandamano dhidi ya serikali tangu mwaka 2014.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yanayashutumu majeshi ya usalama kwa ukiukaji mkubwa, ikiwemo mateso na kuelezewa kuwa takriban watu 400 wameuawa ikiwa ni majibu ya ghasia hizo.
Maelfu ya watu walikamatwa wakati wa kipindi cha miezi 10 ya hali ya dharura ambacho kilifikia hatima yake Agosti mwaka jana.
Kiongozi wa upinzani Merera Gudina, ambaye mpaka hivi karibuni alikuwa miongoni mwa wale ambao walifungwa kutokana na maandamano, ameiambia VOA kuwa kuachia madaraka kwa waziri mkuu hakubadili chochote.
“Hakuna haja ya kusherehekea kwa sababu ni mabadiliko ndani ya chama tawala. Nini ambacho chama tawala inakipanga hatukijui. Waziri mkuu hajawahi kuwa na nguvu kama waziri mkuu wa zamani, kwa hiyo kuna machache sana ya kusherehekea kwa sababu ya mabadiliko yatakayotokea. Kwa kweli, mabadiliko yanaweza kuwa ya kurudi nyuma, hilo ndiyo linatutia wasi wasi. Kuna uwezekano wa kuichukua tena nchi na kuipeleka katika hali ya dharura au chochote kile,” anasema Gudina.
Kwa kweli, maafisa wa chama tawala wameiambia VOA kwamba Baraza la Mawaziri linatarajiwa kutangaza hali ya dharura kwa kipindi cha miezimitatu, huku jeshi likiwa na jukumu mpaka bunge, ambalo liko katika mapumziko , litakaporejea na kuidhinisha kujiuzulu kwa Hailemariam.
Mwezi huu tumeona maandamano mapya, ikiwemo mgomo katika mkoa wa Oromia, ambako kuna vurugu tangu mwaka 2014. Waandamanaji wamekuwa wakidai yafanyike mageuzi ya kisiasa na kiuchumi.
Wachambuzi wanasema kuwa mbinu kali za serikali zimepelekea makundi mengine na maeneo kujiunga katika harakati za upinzani, ingawaje kuna hatua za maridhiano ambazo zinachukuliwa na serikali kama hivi karibuni kuwaachia mamia ya watu waliotiwa ndani kwa mujibu wa sheria ya hali ya dharura.
Gudina anasema madai ya waandamanaji bado ni ile ile, “watu wanataka mabadiliko ya msingi, serikali ya kidemokrasia, uchaguzi huru na wa haki, na taasisi huru za kidemokrasia. Tunaunga mkono madai hayo, lakini tuna wasi wasi chama tawala kinafikiria kufanya nini, hatulijui hilo.”
Waziri mkuu anayeondoka madarakani amejigamba jinsi utawala wake ulivyoshughulikia uchumi wa nchi tangu achukue madaraka mwaka 2012. Ethiopia imeelezewa itakuwa ya pili barani Afrika kwa uchumi unaokuwa haraka mwaka huu wa 2018.
Waziri mkuu atabakia madarakani mpaka bunge litakapothibitisha kujiuzulu kwake.