Shashi Kapoor, mcheza sinema maarufu wa India, afariki

Nyota na Mchezaji filamu mkongwe wa Bollywood Shashi Kapoor (kushoto) akiwa na mzalishaji filamu wa New York Ismail Merchant (kati) na Matthew Modine wakiwa katika picha ya pamoja wakati kuzinduliwa filamu maarufu ya Le Divorce huko Bombay.

Mchezaji na mwongozaji sinema maarufu wa India, Shashi Kapoor, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 79.

Kapoor ambaye alicheza katika sinema nyingi za India zikiwemo filamu maarufu kama vile "Deewar" na "Kabhie Kabhie" amekuwa hospitalini kwa muda mrefu akiuguzwa.

Shashi alikuwa mmoja wa familia maarufu ya Kapoor ambayo imekuwa katika tasnia ya filamu nchini India kwa miaka mingi.

Amewahi kushinda tuzo kadha za filamu na serikali ya India iliwahi kumpa tuzo maalum ya kiraia inayojulikana kama Padma Bhushan hapo mwaka 2011.

Kapoor alianza uchezaji sinema kama mwigizaji mtoto na ripoti zinasema ametokea kwenye filamu zaidi ya 150 ikiwa na pamoja nyingine kadha katika lugha ya kiingereza.

Kapoor alicheza sinema kadha na muigizaji mwingine mkubwa wa India Amitabh Bachchan katika baadhi ya filamu kubwa kubwa kutoka India katika miaka ya 1970 - wakicheza mara nyingine kama ndugu, marafiki na kama maadui.