Wizara ya Mambo ya Ndani ya Yemen inayoshikiliwa na waasi wa Kihouthi imetangaza Jumatatu kwamba Rais wa zamani Ali Abdullah Saleh, ameuliwa na video zimeenea kwenye mitandao ya kijamii zinazo onyesha mwili unaoaminika ni wa kiongozi huyo wa zamani.
Kituo cha televisheni cha Saudi Arabia cha Al Arabia kimewanukuu maafisa wa chama cha rais huyo wa zamani wakithibitisha kifo chake.
Kituo hicho kinaripoti kwamba Ali Saleh aliuawa katika mapigano dhidi ya kundi la wahouthi wanaoungwa mkono na Iran katika mji mkuu wa Sanaa lakini hakuna taarifa zaidi iliyotolewa.
Vifaru vya wapiganaji wa kihouthi vimewekwa katika njia inayoelekea kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sanaa kufuatia habari za kifo cha Ali Saleh.
Wafuasi wa Saleh wanaonekana wamepoteza udhibiti wa mji huo kufuatia mapigano makali ya siku sita licha ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, kwa siku mbili mfululizo.
Kiongozi huyo wa zamani alitangaza mwishoni mwa wiki kwamba anajitoa kutoka katika muungano.
Alikuwa katika juhudi za kuanzisha mazungumzo ya kumaliza vita vya Yemen. Saleh alisema anataka kubadilisha ukurasa katika uhusiano wake na muungano unaongozwa na Saudi Arabia ikiwa hawataacha kuwashambulia raia wenzake wa Yemen.