Haley: Trump ataipiga Syria tena kama kuna ulazima

Balozi Nikki Haley

Balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa anaeleza kuwa iwapo Rais Donald Trump atalazimika kufanya mashambulizi zaidi Syria, rais ataamrisha yafanyike.

“Na hatoishia hapo,” Balozi Nikki Haley ameiambia CNN Jumapili. “Iwapo italazimika afanye mashambulizi zaidi ataamrisha yafanyike.”

Lakini Haley na Waziri wa Mambo ya Nje Rex Tillerson walitoa ishara tofauti juu ya kipaumbele cha kumuondosha madarakani Rais Bashar al-Assad.

“Hakuna njia yoyote mbadala, ambayo itawezesha suluhisho la kisiasa kutokea wakati Assad akiwa bado yuko katika madaraka,” Haley amesema.

“Ukiangalia vitendo vyake, ukiangalia hali halisi, itakuwa vigumu sana kuweza kuwepo serikali yenye amani na utulivu kwa kuwepo Assad.

“Badiliko la utawala ni jambo ambalo tunafikiri lazima litatokea,” amesema balozi huyo.

Lakini Tillerson amesema kukiangamiza kikundi cha Islamic State bado ni jambo muhimu kwenye lengo la Marekani huko Syria.

“Ni muhimu kuweka vipaumbele vyetu imara,” Tillerson ameliambia shirika la habari la CBS katika kipindi cha “Face the Nation.’

“Tunaamini kuwa kipaumbele namba moja ni kuishinda ISIS,” ambayo ni kifupi cha kundi la Islamic State.

“Pale tishio la ISIS likidhibitiwa au kuondolewa,” amesema Tillerson, “nafikiri hapo ndipo tunaweza kuangalia upande wa kuiimarisha hali ya Syria.”

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu kabisa wa Marekani ameongeza kuwa, “ Sisi tunatumaini kuwa tunaweza kuzuia kuendelea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe na tutaweza kuzileta pande zote katika meza ya mazungumzo kuanza mchakato wa mazungumzo ya kisiasa,” kati ya Serikali ya Assad na makundi mbalimbali ya upinzani yanayojaribu kupindua utawala wa Damascus.