Lakini wakati huohuo Wademokrati wanakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa wanaharakati wenye mrengo wa kiliberali kwamba wasimpitishe.
“Tunamatumaini wiki moja baada ya Alhamisi, nitakuwa ninaweza kuwaambia kwamba (Gorsuch) amefanya kazi nzuri katika kujibu maswali (katika mahojiano ya kuthibitishwa) na kwamba mtu yoyote atapata fedheha (kupinga kupitishwa) kwake,” mwenyekiti wa Kamati ya Sheria ya Seneti, Mrepublikan Chuck Grassley wa Iowa, ameiambia VOA. “Nahisi kuwa hivyo ndivyo itakavyo tokea.”
Falsafa za Waconservative
Jaji Gorsuch wa mahakama ya Rufaa aliyekuwa ameteuliwa na Rais mstaafu George W. Bush mwaka 2006, atajaza nafasi ya Mahakama Kuu iliokuwa imeachwa wazi na Jaji Antonin Scalia, ambaye ni Mconservative, aliyefariki mwaka jana.
Kwa wengi Jaji Gorsuch anaonekana ni fasaha na mwenye uwezo anafuata falsafa za kisheria za kiconservative, zinazotokana na maelfu ya kesi za mahakama za serikali kuu kwa zaidi ya muongo moja. Hilo ndilo linalowafanya Wademokrati wawe na wasiwasi.
“Jaji Gorsuch anaweza kuonekana kama msomi, jaji asiye na upendeleo, lakini rikodi zake zinaonyesha kuwa ni wa mrengo wa kulia, mwenye kuyapendelea makampuni ya biashara, na ajenda zenye maslahi maalumu,” amesema kiongozi wa wachache Seneta Chuck Schumer, Mdemokrati anaeiwakilisha New York. “ Rikodi zinaonyesha kuwa Jaji Gorsuch anaupendeleo kwa wakuu wa makampuni kuliko wananchi, wakarugenzi kuliko waajiri, makampuni makubwa kuliko walaji.”
“Haijulikani upande gani Gorsuch anaangukia katika mstari wa majaji maconservative, lakini bila shaka yeye atakuwa ni katika upande wa misamamo wa maconservative,” amesema Profesa Rick Hasen, wa Chuo Kikuu cha California, “Kuna uwezekano mkubwa akawa kama Jaji Kennedy (mwenye msimamo wa kati), lakini akafanya maamuzi kama Jaji Scalia.”