Maafisa wa Marekani waliozungumza na shirika la AP ,Gazeti la New York Times, na Washington Post wamesema kuwa maagizo ya Comey yanafuatia madai ya Trump siku ya Jumamosi kwenye mtandao wake wa Twitter ambao ulijumuisha kufananisha kujiuzulu kwa rais wa zamani Richard Nixon kutokana na kashfa mwaka 1974. Trump hajatoa ushahidi wowote kuhusiana na madai hayo.
Jambo ambalo haliko wazi ni kwa nini Comey hajakanusha hilo yeye mwenyewe. Akiwa Mkurugenzi wa FBI chini ya Obama, idara yake imekuwa ikiongoza katika uchunguzi unaoendelea kuhusu kuingilia kati Russia uchaguzi wa mwaka jana Marekani.
Madai ya Rais Trump ni kuwa Rais mstaafu Barack Obama aliamrisha idara ya upelelezi wa jinai FBI kusikilizwa simu yake katika Jengo la Trump Tower New York.
Gazeti la New York Times na kituo cha televisheni cha NBC vimeripoti kuwa Comey anaamini kwamba madai ya Trump ni ya uongo na tuhuma hizo zinaashiria kwamba FBI ilihusika katika kupanga kusikilizamawasiliano ya simu kinyume cha sheria.
Mpaka hivi sasa Idara ya FBI na wizara ya sheria hawajatoa tamko lolote kuhusu ripoti hizo za vyombo vya habari.