Al Jarreau mwanamuziki mwenye kipaji cha kipekee afariki

Al Jarreau akipokea tuzo yake Grammy kwa nyimbo ya "God Bless the Child" hapo February 11, 2007.

Habari za kifo cha mwanamuziki mashuhuri wa mtindo wa jazz, pop na rhythm na blues, zimetolewa Jumapili saa chache kabla ya kuanza kwa sherehe maarufu na muhimu za muziki Marekani, Grammy Awards.

Al Jerreau ambaye ni mshindi wa tuzo saba za Grammy, alifariki Jumapili akiwa na umri wa miaka 76, katika hospitali mjini Los Angeles, mji unaoanda sherehe hizo kila mwaka. Hata hivyo sababu za kifo chake hazijaelezewa.

Alilazwa hospitali wiki iliyopita kutokana na uchovu, na alipokuwa anapata nafuu pole pole kama ilivyoelezwa kwenye ukurasa wake wa Facebook, alilazimika kufuta maonyesho yake yote ya 2017.

Jarreau, msanii aliyekuwa na kipaji maalum ,alikuwa mojawapo wa wanamuziki wa kipekee kuweza kushinda tuzo ya Grammy katika mitindo mitatu tofauti ya muziki; jazz, pop na rhythm and blues

Alitoa album 16 zilizorikodiwa ndani ya studio na nyingine nyingi wakati wa tamasha za muziki wake. Alichukuliwa kama moja wa waimbaji wakuu wa jazz. Miongoni mwa vibao vyake mashuhuri ni pamoja na "We're in This Love Together," "After All" na "Moonlighting."

Al Jarreau akitumbuiza siku ya Jazz Ufaransa