Rais Magufuli Kuwaapisha Mabalozi Wapya Ikulu Dar es Salaam

Rais John Magufuli

Rais Dkt John Magufuli wa Tanzania amewapangia vituo vya kazi Mabalozi wapya watatu ambao aliwateua tarehe 3 Disemba 2016.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika mabalozi hawa wanategemewa kuapishwa na rais Jumapili, ikulu, Dar es Salaam.

Joseph Sokoine anakuwa Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji na Omar Yussuf Mzee amepangiwa kuwa Balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Algeria.

Balozi Grace Mgavano anakwenda kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Dkt Ladis Komba nchini Uganda ambaye alistaafu kwa mujibu wa sheria.

Balozi Sokoine anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Deodorus Kamala ambaye kwa sasa ni Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kabla ya uteuzi huo Sokoine alikuwa Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Balozi Mzee kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo alishawahi kushika nafasi mbalimbali katika serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nafasi ya mwisho aliyoitumikia Balozi Mzee ni kuwa waziri wa Fedha wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika awamu ya kwanza ya Rais Dkt Ali Mohammed Shein.

Kwa upande wa Balozi Mgavano kabla ya kuteuliwa kushika wadhifa huo alikuwa Afisa Mwandamizi katika Ofisi ya Rais, Ikulu.