Mbilia Bel aibuka na album mpya, asema ni ya mwisho

Mwanamuziki wa Congo Mbilia Bel

Mbali na kusheherekea kuzaliwa kwa kutimiza miaka 57, mwanamuziki huyo Mboyo Moseka, aliyevuma kwa jina la “Mbilia Bel” na kukonga nyoyo za watu wengi ameadhimisha pia miaka 40 ya kuweko kwake katika tasnia ya muziki.

Album yake mpya ya kuwaaga wapenzi wa muziki wake inatarajiwa kutolewa wiki ijayo.

Mwandishi wa idhaa ya Kiswahili VOA Saleh Mwanamilongo amesema kustaafu kwake mwanamke huyu mashuhuri kutoka kwenye tasnia ya muziki, kumekuja mwezi mmoja baada ya kuzuka kwa taarifa kwamba amefariki.

Mbilia Bel

Kwenye kanda ya video ya dakika 5 aliyorikodi, Mbilia Bel amesema kwamba ataendelea kuwa mshauri wa wasichana chipukizi wanawania kuingia katika tasnia ya muziki hivi sasa.

Mwanamuziki Mbilia Bel, alipata sifa kubwa katika miaka ya 70 na thamanini kutokana na sauti yake nyororo.

Lakini hasa baada ya kujiunga na mwanamuziki TabuLey Rochereau. Pamoja na Tabu Ley, supasta huyu alipata umaarufu baada ya kuimba nyimbo nyingi zilitotungwa na Rochereau.

Kwa mfano nyimbo yake ya “Eswi yo wapi” inayomaanisha “kwa nini umekerwa” ikiwa ni wimbo wa fumbo baada ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Rochereau.

Wimbo mwingine maarufu sana nchini ni “yamba ngaa” unaomaanisha “nipokee mpenzi.”

Mbilia Bel na Tabu Ley walizaa mtoto wa kike, Meledoy Tabu ambaye pia ni mwana muziki hivi sasa.

Baada ya kuvunjika kwa uhusiano wake na Tabu Ley, Mbilia Belaliunda bendi yake mwenyewe na kuimba nyimbo nyingi … kama Manzili Manzili kwa lugha yao ya kinyansi, kutoka jimbo la Bandundu kusini magharibi mwa DRC.

Hivi sasa Mbilia Bel amemaliza kurikodi album mpya ambayo inatarajiwa kutolewa wiki ijayo.

Album hiyo mpya anayoita “Signature” au saini ina nyimbo 21.

Katika ukanda wa Afrika mashariki Mbilia Bel ataendelea kumbukwa hasa kutokana na wimbo unaoitwa Nairobi.

Imetayarishwa na mwandishi wetu Saleh Mwanamilongo, DRC