Waendesha mashtaka wa serikali kuu ya Brussels wamesema Jumatatu kwamba wamewafungulia mashtaka watu watatu kwa kuhusika kwao katika kundi moja la ugaidi.
Ukamataji huo unafuatia shambulizi la mabomu wiki iliyopita katika mji mkuu wa Ubelgiji ambalo liliuwa watu wasiopungua 35, wakiwemo raia wanne wa Marekani. Taarifa kutoka kwenye ofisi hiyo imesema kwamba mtu wa nne aliyekamatwa, aliachiwa Jumapili.
Watu hao waliofunguliwa mashtaka wametajwa kuwa ni Yassine A. Mohamed B na Aboubaker O.
Hakuna taarifa zaidi zilizotolewa na waendesha mashtaka hawakusema moja kwa moja kama washukiwa walihusika katika shambulizi la wiki iliyopita lililosababisa vifo.
Wakati huo huo rais wa Marekani Barack Obama alitoa rambi rambi zake Jumapili kwa njia ya simu kwa wazazi wa Justin na Stephanie Shults, wanafamilia ambao walifariki katika mashambulizi ya wiki iliyopita huko Brussels.