Wananchi wa Zanzibar leo wamejitokeza kwa wingi katika uchaguzi mkuu wa marudio wa kumchagua Rais wa Zanzibar, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na Madiwani, huku hali ya amani na utulivu ikiwa imeimarishwa na vikosi vya ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali ya visiwa vya Unguja na Pemba.
Your browser doesn’t support HTML5
Wakati wananchi hao wakijitokeza katika vituo mbalimbali vya kupigia kura, maeneo mbalimbali ya mji wa Zanzibar yametawaliwa na ukimya wa hali ya juu kutokana na wananchi wengi kujifungia majumbani mwao kwa lengo la kujiepusha na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima.
Mgombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM Dk.Ali Mohamed Shein amepiga kura yake katika kituo cha Bungi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja na kupanga foleni kama wananchi wengine kusubiri haki yake ya kupiga kura na kisha kuzungumza kwa ufupi na waandishi wa habari kuhusiana na uchaguzi huo wa marudio.
Aidha, Mgombea Urais wa Chama cha ADA-TADEA Bwana Juma Ali Khatib amesema uchaguzi huo wa marudio umefanyika katika hali ya amani na utulivu lakini amesikitishwa na kitendo cha baadhi ya wananchi kutojitokeza kuchagua viongozi wao kwa sababu mbalimbali.