Kiongozi wa chama cha FDC Dr.Kiza Besigye na uongozi wa juu wa chama chake wamekamatwa na Polisi Ijumaa.
Kukamatwa huko kumefuatia hatua ya kiongozi huyo kuitisha mkutano na waandishi wa habari katika ofisi za chama chake bara bara ya Entebbe.
Lakini kabla mkutano huo kufanyika polisi walivamia eneo hilo na kuwakamata viongozi wa chama hicho pamoja na kurusha gesi za kutoa machozi na huku wakitumia helikopta kumwaga maji yanayowasha.
Helikopta ya polisi iliwasaidia polisi waliokuwa ardhini kwa kunyunyuzia maji ya kuwasha kuwatawanya wafuasi wa Besigye, walianza maandamano moja kwa moja waliposikia kwamba Besigye amekamatwa.
Kutokana na kadhia hiyo Ilibidi wanajeshi kuitwa kuwasaidia polisi kuwatawanya waandamanaji.
Besigye amekamatwa pamoja na kiongozi wa chama cha FDC Meja generali Mugisha Muntu na mkuu wa tume ya uchaguzi wa chama hicho Waswa Birigwa, na kiongozi wa wanawake chamani Ingrid Turinawe.
Polisi walizingira ofisi hizo mda mfupi kabla ya Besigye na viongozi hao wa chama kuanza kuzungumza na waandishi wa habari.