Obama kuwahutubia Wamarekani Jumapili jioni

Rais Obama atalihutubia taifa siku ya Jumapili, Dec. 6, 2015 saa mbili jioni kufuatia kisa cha mauaji kilichotokea mjin San Bernardino siku ya Alhamisi.

Na BMJ Muriithi

White House imesema kwamba rais Barack Obama atalihutubia taifa Jumapili jioni.

Taarifa iliyotolewa kwa waandishi wa habari mjini Washington Jumamosi jioni ilisema kwamba Bw Obama atafanya hotuba hiyo isiyo ya kawaida kufuatia mashambulizi yaliyofanyika mjini San Bernardino katika jimbo la California siku ya Alhamisi.

“Rais Obama atafanya hotuba rasmi kwa taifa kuelezea mikakati iliyowekwa na serikali kuhakikisha kwamba Wamarekani wako salama, jambo ambalo tunalipatia umuhimu mkubwa,” ilisema kauli ya msemaji wa ikulu ya White House, Josh Earnest.

Mashambulizi hayo ambayo yalitekelezwa na mtu na mkewe yaliwaua watu kumi na wanne na kuwaacha wengine 21 wakiwa wamejeruhiwa.

Hii itakuwa ni mara ya tatu tu kwa rais Obama kuhutubia taifa kutoka afisi yake ijulikanayo kama Oval office. Msemaji wa ikulu alisisema ni nadra kwa Obama kulihutubia taifa kutoka afisi hiyo na kwamba yeye hufanya hivyo wakati ana jambo muhimu na la dharura la kuwaeleza wamarekani.

Hotuba yake ya kwanza kutoka Oval office ilikuwa Juni 15, mwaka wa 2010 na ya pili ilikuwa Agosti, 31, 2010.

Idara ya ujasusi ya FBI imesema inalichunguza Shambulio hilo kama la kigaidi.