Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amesema Jumapili Russia inapanga kupiga mabomu Odessa. Zelenskyy alisema katika taarifa iliyotangazwa kupitia televisheni iwapo hilo litatokea, itakuwa, ni uhalifu wa vita … uhalifu wa kihistoria.”
Zelenskyy akizungumza kwa lugha ya Kirusi katika sehemu ya taarifa hiyo, aliwasihi Warussia kuchagua kati ya uhai na utumwa katika “kipindi ambacho bado kuna uwezekano wa kuushinda uovu bila ya hasara isiyoweza kurekebishwa.”
Rais wa Russia Vladimir Putin amesema Jumamosi kuwa taifa la Ukraine liko katika hatari iwapo nchi itaendelea na mwenendo huu wa sasa.
Wakati wa mkutano na wafanyakazi wa Aeroflot, Putin aliongeza kwamba hatua yoyote ya kuweka”marufuku ya safari za ndege” kwenye anga ya Ukraine itakuwa “na matokeo yenye makubwa sana na hasara siyo tu kwa Ulaya bali kwa ulimwengu mzima.”
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ameikosoa NATO kwa kutoweka marufuku ya kutumia anga ya Ukraine, jambo ambalo washirika wa Magharibi wanasema huenda likachochea mzozo na Russia.
Rais wa Marekani Joe Biden alizungumza Jumamosi usiku na Rais wa Ukraine. Walizungumza kuhusu kazi ambayo Marekani, washirika wake, wadau mbalimbali na viwanda binafsi wanafanya kuongeza gharama ya vita kwa Russia.
Biden alisema utawala wake unaimarisha usalama, uchumi na misaada ya kibinadamu kwa ajili ya Ukraine na inafanya kazi na Bunge la Marekani kuongeza msaada wa kifedha.
Zelenskyy mwenyewe alikutana kwa njia ya mtandao mapema Jumamosi na zaidi ya watu 300, wakiwemo maseneta, baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na wasaidizi wao, alitoa “ombi la dharura” kupelekewa ndege zaidi ili kuisaidia nchi hiyo kupambana na uvamizi wa Russia, kwa mujibu wa kiongozi wa Waliowengi katika baraza la Seneti Chuck Schumer.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken alikutana Jumamosi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland Zbigniew Rau mjini Rzeszow, ulioko kwenye mpaka na Ukraine.
Blinken alivuka kuingia Ukraine kwa muda mfupi kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Dymtro Kuleba, aliyeomba wapatiwe msaada wa zaidi wa kijeshi ili kuishinda Russia.
Baada ya kufanya mkutano wa mwenzake wa Poland, Blinken alirejea kusema katika mkutano wa waandishi wa habari kuwa Marekani “itatetea kila inchi ya eneo la NATO” na kutangaza kuwa utawala wa Biden unajitayarisha kutenga dola bilioni 2.75 zaidi kwa ajili ya misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Ukraine.