Akizungumza kwenye mkutano wa uchumi wa dunia kwa njia ya video, Zelensky amesema kuna fursa kubwa ya kumaliza mzozo kati ya Russia na Ukraine ikiwa Putin anaelewa ukweli wa mambo.
Zelensky ameongeza kuwa hatua ya kwanza ili mazungumzo na Russia yafanyike, ni wanajeshi wa Russia kuondoka kwenye mipaka iliyokuwepo kabla ya Russia kuanzisha uvamizi wake mwishoni mwa mwezi Februari.
Huko Russia, Rais Vladimir Putin ametoa amri ambayo itaharakisha mchakato wa kuwapa uraia watu wanaoishi katika maeneo ya Kherson na Zaporizhzhia.
Maafisa wa Ukraine wamesema mapigano ya hivi karibuni kati ya vikosi vya Russia na Ukraine yalifika karibu na mji wa viwanda wa Severodonetsk, wakati wanajeshi wa Moscow wakijaribu kuchukua udhibiti wa eneo la Donbas mashariki mwa Ukraine baada ya kushindwa kumuondoa madarakani Zelensky na kuuteka mji mkuu, Kyiv.