Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 06:34

Zambia na China zakubaliana kurekebisha masharti ya mkopo


Rais wa Zambia Hakainde Hichilema na mwenzake wa China Xi Jinping
Rais wa Zambia Hakainde Hichilema na mwenzake wa China Xi Jinping

Serikali ya Ufaransa imesema kuwa Zambia imefikia makubaliano na China na wakopeshaji wengine kadhaa wa serikali kurekebisha upya masharti ya mikopo ya takriban dola bilioni 6.3.

Mpango huo ulitangazwa pembeni mwa mkutano mkuu mjini Paris, ambao unalenga kuleta mageuzi katika mfumo wa fedha duniani ili kusaidia mataifa yanayoendelea - kama Zambia.

Makubaliano hayo yanahusu mikopo kutoka nchi kadhaa, zikiwemo Ufaransa, Uingereza, Afrika Kusini, Israeli, India na China - mkopeshaji mkuu wa Zambia. Makubaliano hayo, yaliyotangazwa na maafisa waliozungumza bila kutaka majina yao yatajwe, kwa mujibu wa desturi za kitamaduni za serikali ya Ufaransa, huenda yakatoa ramani ya jinsi China itashughulikia mikataba ya urekebishaji upya na mataifa mengine yaliyo katika dhiki ya madeni.

Mfuko wa Fedha wa Kimataifa uliidhinisha mpango huo, ikimaanisha kuwa utairuhusu Zambia kupokea ufadhili zaidi kutoka kwa taasisi hiyo, serikali ya Ufaransa ilisema.

Makubaliano ya Zambia yalikuja katika mkutano wa zaidi ya viongozi 50 wa dunia, maafisa wa taasisi za kifedha, na wanaharakati, kujadili njia za kurekebisha mfumo wa fedha duniani ili kusaidia vyema mataifa yanayoendelea yanayokabiliana na madeni, mabadiliko ya hali ya hewa na umaskini.

Zambia ilishindwa kulipa deni lake hapo mwaka 2020, hali iliyoifanya vigumu kujiendeleza kiuchumi na kuanza miradi mipya. Wataalamu wamesema migogoro hiyo ya muda mrefu ya madeni inaweza kupelekea mataifa kutumbukia katika umaskini na ukosefu wa ajira kwa kuifanya iwe vigumu kupata mikopo ya kujenga kwa ajili ya siku zijazo.

Forum

XS
SM
MD
LG