Elfu kadhaa ya watu walikusanyika mbele ya ofisi ya tume ya kura ya maoni mjini Juba hiyo jana, wakihimili jua kali, ili kumsikiliza mkuu wa tume, Chan Reec Madut, akiwaeleza kwamba kati ya watu millioni 3.8 walopiga kura huko Sudan Kusini, ni watu elfu 16 pekee ndio wanopinga uhuru.
“Wale walopigia kura ya kutaka kujitenga huko Sudan Kusini ni millioni 3, lakin elfu tisiini na saba, mia nne na sitini na saba. Hiyo ikiwa ni asli mia 99.57, alisema Bw. Madut.
Mkuu wa serikali ya ndani ya Sudan kusini, makamu rais wa Sudan, Salva Kiir, alipongeza kura ya maoni kwa kuwa ilifanyika kwa nidhamu na amani.
Akizungumza kwa Kiarabu na Kingereza, aliihimiza Sudan Kusini iwe na subira hadi pale taifa huru litakapo tangazwa rasmi katika muda wa miezi 6, kama inavyohitajiwa kwa mujib wa makubaliano ya mwaka 2005.
“Mulifikiria nitafanya nini hapa? Mulidhani nitatangaza uhuru wa Sudan Kusini? Hatuwezi kufanya hivyo. Lazima tuheshimu makubaliano. Tutakwenda taratibu, ili tuweze kufika kwa salama kule tunakotaka kwenda.” Bw. Kiir alisema.
Alikumbusha tena juu ya ukiukaji wa haki ulofanywa dhidi ya watu wa Sudan Kusini, lakini aliwahimiza wasitende dhulma kama hizo, akiahidi kuweko kwa uhuru na heshima kwa jamii na dini zote.
Bw. Kiir pia alimsifu rais wa Sudan, Omar Al Bashir kwa kuunga mkono uwamuzi wa watu wa Sudan Kusini, na akaahidi kusimama nae bega kwa bega.
Matamshi hayo yametolewa wakati mamia ya wanafunzi walikua wanaandamana huko Khartoum dhidi ya serikali ya Bashir, wakipinga utawala wa kimabavu na bei za juu za vyakula.
Lakini huko Juba, kulikuwa na hali ya sherehe.
Mmoja kati ya walohudhuria sherehe, mfanayakazi wa afya, Thomas Obulejo, alisema watu wanafuraha kwa sababu baada ya zaidi ya miaka 50, wanahisi kwamba wamepata uhuru wao.
“Tumekandamizwa kwa muda mrefu. Hatukuwa na haki zozote. Daima tulikuwa tunanyimwa haki zetu. Tumekuwa tukiishi ndani ya nchi yetu kama watumwa, hamna elimu, hamna huduma za afya, hamna lolote,” amesema Obulejo.
Katika miezi sita ijayo, wakuu wa Kaskazini na Kusini lazima wajadili masuala mengi juu ya kutengana, ikiwa ni pamoja na kuchorwa kwa mpaka, haki za mafuta, na hali ya baadae ya eneo la Abyei.
Lakini wengi wanaamini wakati wa kusheherekea umewadia.
Matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa wiki ijayo.