AFRIKA KUSINI.
Wenyeji Afrika Kusini wapo kundi A la mashindano haya ambayo yanafanyika katika ardhi yake na ardhi ya Afrika kwa mara ya kwanza. Taifa hili mwenyeji lipo pamoja na timu za Mexico, Uruguay na Ufaransa katika kundi hili la A inajiandaa kuandika historia katika kipindi kifupi tuu cha historia ya soka katika taifa hili.
Katika miaka ya karibuni Afrika Kusini maarufu kama Bafana Bafana ama wavulana wameonyesha kuwa wanaweza kuwa tishio katika siku za karibuni na kutokana na hamasa kubwa ya mashabiki na serikali wanaweza kutoa changamoto kubwa katika mashindano hayo.
Mwaka 1996, miaka minne baada ya kurejeshwa katika ramani ya soka duniani Afrika Kusini iliwashangaza watu baada ya kutwaa ubingwa wa kombe la mataifa barani Afrika baada ya kuifunga Tunisia katika fainali mjini Johannesburg. Miaka 16 baada ya tukio hilo Afrika Kusini inarejea viwanjani lakini mara hii ikiwa katika ardhi yake ikiwania ubingwa wa kombe la Dunia.
WALIVYOFUZU.
Afrika Kusini kutokana na kuwa muandaaji wa fainali hizi wameingia moja kwa moja kama ilivyo ada ya timu mwenyeji kutotoa jasho.
Wachezaji nyota.
Mchezaji wa kiungo wa Everton ya Uingereza Steven Pienaar ni mmoja wa wachezaji tegemeo kubwa kwa nchi hii. Kukosekana kwa mshambuliaji mahiri, Benni McCarthy, Pinaar amekuwa tegemeo kubwa kwa Afrika Kusini na kama kocha atamwita Benny katika fainali hizi watakuwa na mchango mkubwa kwa Bafana Bafana. Pamoja na Pinaar lakini pia wapo Siboniso Gaxa na Tsepho Masilela ambao pia ni hatari.
REKODI
Hii ni mara ya tatu kwa Afrika Kusini kushiriki katika fainali hizi za FIFA za kombe la dunia.
Mara ya kwanza wameshiriki nchini Ufaransa mwaka 1998 na Korea/Japan 2002.
Benni McCarthy ndiye alikuwa mchezaji wa kwanza wa Afrika Kusini kufunga bao la kwanza la nchi hiyo katika fainali za kombe la dunia mwaka 1998 katika mchezo ambao walitoka sare ya bao moja kwa moja na Denmark.
Kocha: Carlos Alberto Parreira kutoka Brazil.
IVORY COAST
Ivory Coast ipo katika kundi la G pamoja na Brazil, Ureno, na Korea ya Kaskazini.
Kama kuna tmu ya Afrika inaweza kutoa changamoto kubwa katika mashindano ya fainali za kombe la dunia mwaka huu nchini Afrika Kusini basi ni Ivory Coast. Na kwa jinsi timu hii ilivyo na vipaji kuanzia namba moja hadi kumi na moja haitakuwa ajabu. Baada ya kuondolewa katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani kwa kufungwa mabao 2-1 na Argentina na Uholanzi kabla ya kuifunga Serbia mabao 3-2.
Timu hii sasa ina uzoefu wa kutosha na imepata bahati kidogo katika kundi lake ni matarajio ya wengi kuwa Didier Drogba na wenzake watafanya vizuri katika mashindano haya ya Afrika Kusini mwaka huu 2010.
WALIVYOFUZA.
Ivory Coast walivuka kundi lao kwa kishindo wakiwapita Burkina Faso, Malawi na Guinea.Na hata walipohitaji pinti moja tuu ili wafuzu Didier Drogba akitokea wachezaji wa akiba alifunga bao dhidi ya Malawi na kufuzu.
Wachezaji nyota.
Ivory Coast ama tembo wana wachezaji nyota wengi lakini wengi wanawatupia macho Didier Drogba na Salomon Kalou wa Chelsea na katikati yupo kiungo wa Sevilla ya Uhispania Didier Zokora Yaya Toure wa Barcelona, bila kumsahau Bakary Kone wa Marseille ya Ufaransa na Emmanuel Eboue wa Arsenal na Kolo Toure wa Manchester City na mlinzi wa Stuttgart Arthur Boka
Kocha: Sven-Goran Eriksson wa Sweden.
REKODI.
Ivory Coast ndiyo timu pekee ya Afrika ambayo haijawahi kutoka uwanjani bila kufunga bao katika mashindano yanayoandaliwa na FIFA.
CAMEROON
Cameroon ipo katika kundi la E lenye timu za Uholanzi, Denmark na Japan.
Licha ya kwamba umaarufu wa Cameroon umepungua baada ya kug’hara katika fainali za kombe la dunia za mwaka 1990, Cameroon Cameroon sio timu ya kuipuuza hata kidogo katika fainali za mwaka huu za Afrika Kusini. Cameroon ambayo imekuwa katika kiwango bora cha FIFA kwa Afrika lakini pia imeshiriki fainali hizo mara nyingi zaidi kuliko taifa jingine la Afrika. Lakini pia hakuna timu ya Afrika iliyowahi kufikia rekodi yake kufikia robo fainali mwaka 1990 licha ya kwamba Senegal imefikia rekodo hiyo mwaka 2002.
Lakini Cameroon haijawahi kuvuka hatua ya makundi katika fainali tatu ilizoshiriki ikishinda mechi moja tu kati ya tisa ilizocheza.
Hawakushiriki fainali za 2006 nchini Ujerumani lakini kufuzu kwa fainali hizi za Afrika Kusini Wacameroon wengi wanaamini kuwa ni kuwepo kwa mchanganyiko wa wachezaji wazoefu na wachanga ambao sasa wanatoa damu itakayorithi kizazi cha akina Roger Millas na Francois Omam-Biyiks.
WALIVYOFUZU.
Cameroon walifuzu baada ya kuifunga Morocco mabao 2-0 na kupata tiketi ya kwenda Afrika Kusini. Cameroon walianza kwa kutoka sare mechi za o mbili za awali. Cameroon walifanikiwa kuziacha Togo , Gabon na Morocco .
Timu hiyo inaundwa na wachezaji wazoefu kama Geremi Njitap, Rigobert Song na mlinda mlango Idriss Carlos Kameni,ambaye aliruhusu nyavu zake kutikiswamara mbili tuu katika michezo sita.
WACHEZAJI NYOTA
Samwel Eto'o amefunga magoli 9 katika michezo 11 ya kufuzu kwa timu hiyo akifuatiwa na Pierre Webó huku Jean Makoun, Stephane Mbia na Alexandre Song wakimiliki sehemu ya katikati na kuwalinda mabeki Rigobert Song, Geremi na Kameni.
Kocha: Mfaransa Paul Le Guen.
REKODI.
Cameroon iliondolewa katika hatua ya makundi nchini Spain mwaka 1982 na imecheza mechi kumi na saba zinazoandaliwa na FIFA ikiwa ni zaidi ya taifa lolote la Afrika. Roger Milla aliandika rekodi ya kuwa mchezaji aliyeshiriki fainali za kombe la dunia akiwa na umri wa miaka 42 na siku 39 alipofunga bao dhidi ya Russia katika fainali za mwaka 1994.