Wizara ya afya ya Uganda ilithibitisha Alhamis mtoto wa kike mwenye umri wa miaka tisa aliyevuka mpaka kutoka Kongo na kuingia Uganda ameambukizwa virusi vya Ebola. Mtoto huyo anapatiwa matibabu kwa wakati huu katika kituo maalumu cha kupambana na Ebola katika wilaya ya Kasese.
Imeripotiwa mtoto huyo alikuwa na dalili za homa kali, pamoja na udhaifu wa mwili, vipele na damu kutoka mdomoni bila ya kufahamu sababu zake.
Damu yake ilipimwa katika taasisi ya utafiti wa virusi vya Ebola ya Uganda na baadae taasisi hiyo ilithibitisha alikuwa na virusi hivyo.
Dr. Joyce Moricu Kaducu alisema binti huyo haraka aliwekwa kwenye chumba cha peke yake na alisafirishwa hadi hospitali ya Bwera kwenye kitengo cha Ebola mahala ambako anapatiwa huduma maalum.
Hii ni mara ya pili kesi ya Ebola imethibitishwa nchini Uganda kutoka kwa waathirika wanaovuka mpaka kutoka Congo kuingia Uganda. Zaidi ya watu 1,800 wamekufa nchini Congo kutokana na ugonjwa huo tangu Agosti 2018.
Wizara ya afya ya Uganda hivi sasa inarudia kutoa wito kwa raia wake kushirikiana na wafanyakazi wa afya, maafisa wa uhamiaji na polisi kuhakikisha ukaguzi unafanyika kwenye vituo vyote vya kuingilia mipakani ili kuzuia kusambaa ugonjwa wa Ebola nchini humo. .
Kesi hii imetokea wakati ambapo chanjo ya majaribio ya Ebola ikiendelea kutolewa na wanasayansi nchini Uganda katika juhudi za kuzuia ugonjwa kutosambaa sehemu nyingine. Chanjo hiyo mpya imetengenezwa na kiwanda cha madawa Janseen Pharmaceutical chenye makao yake nchini Marekani.
Majaribio ya chanjo yanatarajiwa kudumu kwa miaka miwili na kuhudumia zaidi ya watu 800 katika wilaya ya Mbarara huko kusini magharibi mwa Uganda.