Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 24, 2025 Local time: 06:35

Waziri wa usalama wa Kenya, Joseph Nkaissery, afariki ghafla Nairobi


Meja Jenerali Joseph Nkaissery. Aliaga dunia Jumaqmosi tarehe 8/7/2017.
Meja Jenerali Joseph Nkaissery. Aliaga dunia Jumaqmosi tarehe 8/7/2017.

Waziri wa usalama wa ndani nchini Kenya, Meja Jenerali mstaafu Joseph Nkaissery, aliaga dunia Jumamosi  asubuhi katika hospitali ya Karen, kilomita chache kutoka mjini Nairobi.

Afisa mmoja katika ikulu ya Nairobi ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu hana idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari aliiambia Sauti ya Amerika kwa njia simu kwamba Nkaissery alikuwa ameenda hospitalini ili kukaguliwa na madaktari na wauguzi.

Hata hivyo, afisa huyo hakutoa habari zaidi juu ya kile kilichosababisha kifo chake.

Baadaye, mkuu wa watumishi wa umma na katibu wa baraza la mawaziri, Joseph Kinyua, alitoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kuthibitisha kifo cha waziri huyo.

Rais Uhuru Kenyaata wa Kenya na kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, walikuwa kati ya viongozi wa kwanza kuelezea kushangazwa kwao na kifo hicho cha ghafla.

"Nimempoteza rafiki na mfanya kazi shupavu wa serikali," alisema Kenyatta katika hotuba ya rambirambi kutoka ikulu ya Nairobi na ambayo ilipeperushwa moja kwa moja na runinga za Kenya.

Odinga alisema kuwa licha ya tofauti za kisiasa, yeye na Nkaisssery walikuwa marafiki.

"Alikuwa mtumishi shupavu hata alipohudumu kama mwanachama wa ODM," alisema Raila akiwa mjini Mombasa Jjumamosi.

Kabla ya Nkaissery kulalamika kwamba hakuwa anajihisi vizuri, alikuwa ameandamana na rais Uhuru Kenyatta wakati wa mkutano wa maombi ya kitaifa uliofanyika kwenye bustani za Uhuru Park Ijumaa.

"Alionekana mwenye afya nzuri lakini baadaye tukasikia alipelekwa hospitalini kwa ukaguzi," mtu mmoja ambaye hakutambulishwa, amenukuliwa na gazeti la Daily Nation akisema.

Nkaissery aliteuliwa kama waziri wa uslama wa ndani mnamo tarehe 2 Desemba 2014, kuchukua nafasi ya mtangulizi wake Joseph Ole Lenku.

Kabla ya uteuzi huo, alikuwa mbunge wa chama cha upinzani, ODM, akiwakilisha eneo bunge la Kajiado ya Kati.

Alichaguliwa kama mbunge mnao mwaka wa 2002 baada ya kustaafu kutoka kwa jeshi la Kenya alilokuwa amehudumia tangu 1973..

Baada ya kifo chake kuthibitishwa, mwili wa marehemu ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee Funeral Home, ambako jamaa na marafiki walionekana kuwasili wakiwa na majonzi asubuhi ya Jumamosi.

Amefariki akiwa na umri wa miaka 68.

Habari zaidi zitafuata...

XS
SM
MD
LG