Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Desemba 25, 2024 Local time: 08:03

Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss amejiuzulu


Waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss
Waziri mkuu wa Uingereza Liz Truss

Waziri Mkuu wa Uingereza Liz Truss amejiuzulu kama kiongozi wa chama cha Conservative.

Katika hotuba fupi, Truss amesema inabidi kuondoka madarakani kwa ajili ya umoja wa chama chake cha Conservative kwa maslahi ya taifa.

Amekabiliwa na shinkizo kubwa kutoka ndani ya chama cha Conservative kufuatia sera ya kiuchumi ambayo imekosolewa sana.

Kujiuzulu kwake kumetokea muda mfupi baada ya kujiuzulu kwa waziri wa mambo ya ndani Suella Braverman.

Ataendelea kuwa waziri mkuu hadi chama cha Conservative kitakapomteua kiongozi mwingine. Amekuwa madarakani kwa kipindi cha siku 45.

Amesema kwamba wakati chama cha Conservative kinamtafuta mrithi wake, ataendeela kutekeleza sera za kiuchumi kwa ajili ya taifa.

Mpango wake wa kupunguza bajeti ulitikisa soko la fedha na kupelekea chama chake cha Conservative kumshinkiza kuondoka madarakani.

Katika taarifa fupi, Truss amesema, “Tulikuwa na nia ya kuweka kiwango cha chini cha kodi, na kuimarisha ukuaji wa uchumi ili kuifanya Uingereza kuwa na ushindani mkubwa baada ya kuondoka Umoja wa Ulaya.”

“Natambua kwamba kulingana na hali ilivyo, siwezi kutekeleza kazi yangu ipasavyo kulingana na ahadi nilizotoa na matarajio ya chama cha Conservative. Kwa hivyo, nimezungumza na mfalme, na sasa natangaza kwamba najiuzulu kama kiongozi wa chama cha Conservative.”

Kabla ya kujiuzulu, Truss amefanya mkutano na kiongozi Graham Brady, anayesimamia maswala ya siasa kuhusiana na uongozi na mabadiliko ndani ya chama.

Brady ni mwenyekiti wa kundi la wabunge wa Conservative wasiokuwa na nafasi za uwaziri, na ambao wanaweza kuwasilisha barua za kutokuwa na imani na waziri mkuu.

Kabla ya kujiuzulu, wabunge 17 walikuwa tayari wamesema kwamba wanamtaka Liz Truss ajiuzulu, na wabunge 100 walikuwa wameandika barua kwa kamati ya Brady wakisema hawana Imani naye na ni lazima ajiuzulu.

XS
SM
MD
LG