Waziri Mkuu wa Ugiriki George Papandreou amekubali kujiuzulu ili kuwe na serikali ya mpito ya mseto itakayokuwa na jukumu la kufikia makubaliano na Jumuiya ya Ulaya katika mkataba wa kuondolewa mzigo wake wa deni.
Bwana Papandreou ambaye ana msimamo wa kisoshialisti alikutana Jumapili na kiongozi wa chama cha upinzani cha New Democratic Party Antonis Samara. Serikali mpya ya mseto inatazamiwa kuongoza Ugiriki hadi uchaguzi mkuu mwezi Machi.
Pande zote zitakutana tena Jumatatu kukubaliana juu ya nani atakayeongoza serikali hiyo ya mseto. Lengo la kuwa na serikali ya muda ni kuliwezesha bunge la Ugiriki na baraza la mawaziri kukubali masharti ya msamaha mpya wa deni kutoka kwa Jumuiya ya Ulaya.
Mkataba huo unaitaka Ugiriki kuongeza kiwango cha kodi na kupunguza kwa kiwango kikubwa matumizi katika ajira za serikali na malipo ya uzeeni.
Mzozo wa kisiasa wa Ugiriki ulichochewa na tangazo la kushtukiza kutoka kwa bwana Papandreou kuwa angeomba kuwe na kura ya maoni juu ya masharti ya mkataba wa Jumuiya ya Ulaya. Pendekezo hilo lilishtua wote, jumuiya ya Ulaya na taifa la Ugiriki.