Hatua ya Hicehm Mechichi, huenda ikamuweka katika hali ya mvutano na chama cha Ennahda chenye wabunge wengi na ambacho tayari kimesema kwamba kitapinga kabisa hatua yoyote ya kuteua serikalini watu ambao sio wanasiasa.
Hata hivyo pendekezo la kuunda serikali ya wataalam wasioegemea kundi lolote la kisiasa huenda likapata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa muungano wa wafanyakazi wenye nguvu sana nchini Tunisia -UGTT, Pamoja na vyama vingine vya kisiasa, vikiwemo Tahya Tounes na Dustoury el Hor.
Mechichi amesema kwamba lengo la serikali litakuwa kutatua hali ngumu ya maisha wanaopitia watu wa kawaida na kujenga uchumi ambao umeharibika.
Amekashifu wanasiasa kwa kuzozana wakati raia wa kawaida hata hawana maji safi ya kunywa.
Maandamano yametokea katikati mwa Tunisia mwaka huu kulalamikia ukosefu wa ajira na huduma mbovu serikalini hasa za afya, ukosefu wa maji na umeme.
-Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC