Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 17:44

Waziri Uganda atuma barua ya malalamiko dhidi ya maafisa usalama


Bobi Wine
Bobi Wine

Waziri wa haki na masuala ya katiba Jenerali Kahinda Otafire, amemwandikia barua mwenzake wa maswala ya ndani Jeje Odongo, akilalamikia mwenendo wa maafisa wa usalama akisema tabia yao ni uvunjaji mkubwa wa sheria na vitendo vyao vinakiuka haki za kibinadamu.

“Inaonekana kama kuna mpangilio Fulani wa matumizi ya nguvu na ukandamizaji wa haki za kibinadamu kwa kutumia vibaya madaraka na dhuluma dhidi ya raia” ameandika Jenerali Otafiire.

Umoja wa Mataifa

Tume ya Umoja wa Mataifa kuhusu haki za kibinadamu nayo inataka serikali ya Uganda kuruhusu uchunguzi huru usioegemea upande wowote kutokana na ukandamizaji wa haki za kibinadamu kufuatia vurugu za terehe 13 mwezi Agosti mjini Arua.

Pia inataka serikali kuwafunguliwa mashtaka wahusika wote, Kamishna mkuu wa haki za kibinadamu katika Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad al Hussein akisema kwamba umoja wa mataifa umesikitishwa sana na matukio nchini Uganda.

Malalamiko dhidi ya serikali

Waziri Otafiire, ametaja matumizi mabaya ya ofisi, madaraka, kuwatisha watu, kuwapiga wabunge, kuwateka nyara watu, kuunda ushahidi wa uongo, uchunguzi usio na msingi, kuwalaghai raia, miongoni mwa mengine kuwa tabia inayovunja moyo na isiyoweza kuendelea kuvumiliwa.

Amemtaka waziri mwenzake kuchukua hatua za haraka kuleta nidhamu katika taasisi hiyo ya usalama.

“kuna ongezeko la malalamiko dhidi ya maafisa wa usalama wakishirikiana na maafisa wengine serikalini, kuhusiana na ukamataji, kutishia raia, ulaghai na kutengeneza ushahidi wa uongo dhidi ya washukiwa, “ ameendelea kuandika Waziri Otafiire.

Msimamo wa Waziri wa Usalama

Lakini Waziri wa Usalama Elly Tumwine, amesema kuwa vyombo vya usalama haviwezi kuvumilia watu wanaotaka kuvuruga usalama wa nchi.

Waziri Tumwine ameonya : "Mkitaka kujaribu kuipindua serikali, sisi tupo tayari. Tumechunguza jumbe zote kwenye mitandao ya kijamii, chanzo chake ni nchi za nje kama wakenya wanaofanya maandamano.

Wakenya wana matatizo ya kutosha wanayostahili kuandamana huko sio kuingilia mambo yetu. Tuna ushahidi kwamba mashirika yasiyo ya kiserikali yanatumika kutuvuruga kwa kulipa vyombo vya habari, vijana na wanasiasa."

Spika wa Bunge

Barua ya Waziri Otafiire kwa Waziri Odong, inajiri siku tatu baada ya Spika wa Bunge la taifa Rebecca Kadaaga, kumuandikia barua Rais Yoweri Museveni akitaka maelezo ya kuridhisha, mbona maafisa waliohusika katika kuwapiga risasi na kuua raia hawajakamtwa. Kadaaga, amesitisha shughuli zote za buneg hadi atakapojibiwa.

Maadui wa Uganda

Lakini Waziri wa Usalama anadai kwamba maadui wa Uganda wanawatumia vijana kuvuruga usalama wa taifa na kwamba serikali ya Museveni iko tayari kwa wale wanaotaka kupindua utawala uliopo.

Wakati huo huo, mbunge Francis Zaake aliyepigwa na kujeruhiwa vibaya na maafisa wa jeshi, amezuiliwa katika uwanja wa ndege wa Entebbe akiwa kwenye kitanda cha wagonjwa mahtuti, akiwa anapelekwa nchini India kwa matibabu maalum. Naye Bobi Wine, amelazwa katika hospitali ya Rubaga jijini Kampala.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC.

XS
SM
MD
LG