Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Desemba 27, 2024 Local time: 03:52

Watuhumiwa wa ajali ya meli ya Zanzibar wapewa dhamana


Rais Dk. Ali M Shein akiwafariji walonusurika
Rais Dk. Ali M Shein akiwafariji walonusurika

Watuhumiwa hao, Ijumaa iliyopita walirejeshwa rumande baada ya kuzuka mabishano ya kisheria ya kutaka wapewe dhamana ama wasipewe

Watuhumiwa watatu kati ya wanne waliofikishwa kwenye Mahakama Kuu Mjini Zanzibar wiki iliyopita wakikabiliwa na kosa la uzembe na kusababisha vifo vya watu 203 waliokuwa wakisafiri kwa Meli ya MV Spice Islander na kuzama katika bahari ya Hindi, Septemba 10 2011, wamepewa dhana na haikutaja siku ya kurejea tena Mahakamani hapo.

Watuhumiwa waliopewa dhamana ni Abdallah Mohammed Ali mkazi wa Bububu, ambaye ni Afisa Mkuu wa Meli ya MV Spice Islander, Yussuf Suleiman Jussa mkazi wa Kikwajuni ambaye pia ni Mmoja wa Wamiliki wa Meli na Msimamizi Mkuu wa Mizigo katika meli hiyo na Simai Nyange Simai mkazi wa Mkele, ambaye ni Mfanyakazi wa Mamlaka ya Mamlaka ya Usafiri Baharini anayehusika na usalama wa abiria melini.

Watuhumiwa hao, Ijumaa iliyopita walirejeshwa rumande baada ya kuzuka mabishano ya kisheria ya kutaka wapewe dhamana ama wasipewe, ambapo Msajili wa Mahakama Kuu Zanzibar Mh. George Kazi, aliamuru warejeshwe rumande hadi leo Jumatatu atakapotoa uwamuzi wake.

Walipofikishwa Mahakamani hapo hii jumatatu, Wakili wa Utetezi Bw. Hamidi Ali Saidi Mbwezeleni aliiomba Mahakama iwaachie huru watuhumiwa hao ili tume iliyoteuliwa na Rais kuchunguza chanzo cha kuzama kwa meli hiyo iendelee na kazi yake la sivyo tume isitishe kazi yake hadi pale kesi itakapomalizika.

Wakili huyo amesema kuwa kutakuwa na utata kama watuhumiwa wataendelea kubaki rumande kwani watakosa haki yao ya msingi katika tume iliyoundwa na Rais wa Zanzibar wakati ikiendelea na kazi yake endepo itataka kupata taarifa ama maoni kutoka kwa watuhumiwa hao hivyo wakiwa mahabusu watakosa haki yao ya kujieleza mbele ya tume hiyo.

Amesema hivi sasa inaonekana kuna makundi mawili yanayofanya kazi moja kwa maana ya Mahakama na Tume jambo ambalo alisema litakuwa na utata na lenye makusudio ya kuwalinda baadhi ya watu fulani.

Hata hivyo, ingawa Mwanasheria wa Serikali Ramadhani Ali Nassib alitetea uwamuzi wa kutaka watuhumiwa hao wabaki rumande wakati tume ikiendelea na kazi yake lakini Mh. Kazi alikubaliana na hoja ya upande wa utetezi na kuamuru watuhumiwa hao wawe nje kwa dhamana hadi pale tume ya Rais itakapomaliza kazi yake.

Watuhumiwa wote watatu walipewa dhamana ya maandishi ya shilingi milioni kumi na wadhamini wawili kila mmoja kwa kiasi hichohicho na watuhumiwa hao waliondoka huku mtuhumiwa wa kwanza katika kesi hiyo Saidi Abdallah Kinyanyite ambaye alikuwa Nahodha wa Meli ya Spice Islander akiendelea kusakwa na Polisi.

Ijumaa iliyopita watuhumiwa hao walifikishwa Mahakamani na kusomewa shitaka la uzembe wa kusababisha vifo kwa watu 203 waliokuwa kwenye Meli hiyo na Mh. Kazi alisema hataki kukurupuka kutoa dhamana kwa vile kesi hiyo ina unyeti wake.

XS
SM
MD
LG