Shambulio hilo la waasi wa Alliance Democratic Forces (ADF) la Jumamosi usiku linajiri baada siku mbili tu baada ya kufanyika shambulio kama hilo katika mkoa jirani na kusababisha vifo vya watu 13.
“Majira ya saa tatu usiku, walishambulia kijiji cha Busiyo katika mkoa wa Ituri, na kuchoma nyumba kadhaa, Jacques Anayeyi, kiongozi wa baraza la vijana, ameiambia AFP Jumapili.
Amesema watu watano waliuawa, wakiwemo watoto wanne kutoka familia moja ambao walichomwa hadi kufa ndani ya nyumba yao.
Ameongeza kuwa wanavijiji watano walijeruhiwa na darzeni ya wengine kutekwa nyara.
Shambulio hilo limetokea wakati viongozi walikuwa wanatarajia kuwarejesha makwao wakazi baada ya kuzuka kwa machafuko katika eneo hilo.
“Tulikuwa tumewatayarisha wakazi warejee makwao, lakini kutokana na shambulio jingine la magaidi wa ADF, kurejea itakuwa vigumu,” amesema Faustin Babanilao Mboma, kiongozi wa eneo la utawala la Banyali Tchabi, akithibitisha vifo hivyo.
Waasi hao walishambulia kijiji jirani siku ya Alhamisi, na kuua watu wawili na kuteka nyara 40 wengine, Anayeyi amesema.