Watu watano walifariki baada ya mtu mmoja mwenye bunduki kufyatua risasi kwenye ofisi za gazeti la Capitol Gazette katika mji wa Annapolisi kwenye jimbo la Maryland nchini Marekani. Maafisa wa polisi walisema baadhi ya waathirika walijeruhiwa vibaya na mshukiwa wa tukio hilo yupo kizuizini.
Mashahidi walisema mtu huyo mwenye bunduki alifyatua risasi kupitia mlango wa kioo kwenye ofisi za Capitol Gazette majira ya saa tisa mchana kwa saa za Washington DC na kisha aliendelea kuwashambulia wafanyakazi kwenye chumba cha habari. Ripota mmoja ambaye alikuwa akifanya kazi wakati tukio linatokea, baadae aliandika kwenye ukurasa wa mtandao kwamba yeye alijificha chini ya dawati lake na alimsikia mfyatuaji risasi akifyatua risasi na kuongeza nyingine.
Polisi walisema wanamhoji mshukiwa, lakini chanzo kilichopelekea tukio hilo kutokea bado hakijajulikana.Rais Trump aliandika kwenye mtandao kwamba alipewa taarifa juu ya ufyatuaji risasi huo wakati akirejea mjini Washington kutoka ziara yake ya Wisconsin na alisema sala zake ziwafikia waathirika na familia zao.
Gavana wa jimbo la Maryland Larry Hogan aliandika kwenye ukurasa wa mtandao kwamba alihuzunishwa na tukio hilo lililotokea kwenye mji mkuu wa jimbo lake la Maryland.