Waziri Mkuu Saleh Kebzabo, ambaye alitoa idadi ya waliouawa katika mkutano na waandishi wa habari, alisema serikali bado inakusanya idadi ya majeruhi kutokana na kile alichokitaja kuwa ni uasi wa kutumia silaha.
Lakini mashirika ya kutetea haki za binadamu yalisema kuwa raia wasiokuwa na silaha waliuawa huku vikosi vya usalama vikikabiliana kikatili na maandamano katika mji mkuu wa N'Djamena na miji mingine kadhaa.
Taifa hilo kubwa la Afrika ya Kati linalotawaliwa na jeshi limekuwa katika mgogoro tangu kifo cha Aprili 2021 cha Rais Idriss Deby, ambaye alitawala kwa mkono wa chuma kwa miongo mitatu.
Mtoto wake wa kiume, Mahamat Idriss Deby, alinyakua madaraka mara moja na awali aliahidi kipindi cha mpito cha miezi 18 kuelekea uchaguzi, lakini Oktoba mosi alitangaza kwamba watasogeza mbele kwa miaka miwili.