Zelenskiy alikuwa ameonya Jumanne juu ya hatari ya “uchokozi wa kuchukiza wa Russia” katika siku ya uhuru, ambayo kwa bahati imeadhimishwa miezi sita tangu vikosi vya Russia kuivamia Ukraine, na kuufanya mzozo huo kuwa mbaya zaidi barani Ulaya tangu vita vya pili vya dunia.
Katika hotuba yake kwa njia ya video kwa Baraza la usalama la Umoja wa mataifa, Zelenskiy amesema treni imeshambuliwa na roketi katika mji mdogo wa Chaplyne, umbali wa kilomita 145 magharibi mwa eneo linalokaliwa na Russia la Donetsk mashariki mwa Ukraine. Amesema mabehewa manne yaliteketea kwa moto.
“Chaplyne ni maumivu yetu leo. Kufikia sasa, kuna watu 22 waliokufa,” Zelenskiy amesema katika hotuba ya jioni, akiongeza kuwa Ukraine itaifanya Russia kuwajibika kwa kila kitu ilichofanya.
Hayo yakiarifiwa, Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza msaada wa kijeshi wa dola bilioni 3 kwa Ukraine wakati nchi hiyo ikiadhimisha uhuru wake jana Jumatano, ukiwa msaada mkubwa wa Washington tangu uvamizi wa Russia miezi sita iliyopita, lakini msaada huo utachukua miezi au miaka kadhaa kabla ya kuwasili mjini Kyiv.