Ndege moja ya Umoja wa Mataifa imepata ajali wakati ikitua uwanja wa kimataifa wa Ndjili mjini Kinshasa Jumatatu katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kuuwa watu 16 .
Ndege hiyo aina ya Boeng 727 ilikuwa ikitokea Kisangani katika jimbo la Oriental .
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa nane mchana kwa saa za Kinshasa wakati ndege ilipojaribu kutua kukiwa na mvua hivyo kugonga katika njia zake na kupasuka vipande vipande.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema ndege hiyo ilikuwa imebeba abiria 29 wakati ilipoanguka. Msemaji wa Umoja wa Mataifa kutoka New York amesema kundi la uokozi linafanya kazi katika eneo la tukio.