Mkoa wa Kasai huko Jamhuri ya Kidemocrasi ya Congo-DRC ndio eneo la karibuni la mauaji mabaya katika nchi hiyo ya Afrika ya kati ambayo imekumbwa na uwasi kwa miongo kadhaa.
Kwa mara nyingine watoto ndio miongoni mwa waathirika walio katika mazingira hatari. Kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press-AP zaidi ya watu milioni moja wamekimbia mapigano ambayo yalianza mwaka mmoja uliopita wakati jeshi la Congo lilipomuuwa kiongozi wa kikabila wa wanamgambo wa Kamwina Nsapu. Zaidi ya watu 3,300 katika eneo wamekufa kwa mujibu wa makadirio yaliyofanywa na kanisa la katoliki.
Umoja wa Mataifa ulihesabu zaidi ya makaburi ya 80 ya jumla. Katika eneo zima ambalo liliwahi kuwa na amani, watoto wanalazimishwa kushika silaha, ama wanaandikishwa na wanamgambo au kuzilinda nyumba zao.
Watoto ni zaidi ya nusu ya watu waliokoseshwa makazi alisema Yvon Edoumou, msemaji wa ofisi ya kibinadamu katika Umoja wa Mataifa nchini Congo.