Zawadi ya Santa ilitua mapema kwa familia 27 katika hospitali ya Pumwani katikati mwa jiji kuu Nairobi, kufuatia wanawake 27 kujifumngua siku ya Krismasi.
Miongoni mwa kina mama waliobahatika kujifungua siku hii ya krismasi ni Lilian Syombua mama wa umri wa miaka 34. Alijifungua muda wa saa sita na dakika nane usiku, mwanawe akiwa na uzito wa kilo 2.8.
“Sikutarajia nitajifungua leo, kulingana na hesabu yangu na ratiba yangu ya kliniki nilipaswa kujifungua tarehe 11 Januari mwaka ujao,” alisema Syombua.
Syombua ambaye tayari ana watoto wa tatu wa kike anasema alitamani sana kujifungua mtoto wa kiume na ombi lake limesikika kupitia uzao huu wa siku hii ya krismasi na anasema mwanawe kuzaliwa mapema, hana tatizo lolote la kiafya.
“Bado sijampa jina namsubiri babake aje hospitali, ila kama ni uamuzi wangu ningemuita Emanuel.”
Kulingana na usimamizi wa hospitali hiyo kati ya watoto 27 waliozaliwa 17 ni watoto wa kike na 10 ni wa kiume.
Aidha kulingana na muuguzi msimamizi watoto hawa wamezaliwa na kina mama walio kati ya umri wa miaka 16 na 37.
Yakijiri haya baadhi ya wenyeji wa Nairobi wamejitokeza kusherekea siku hii katika maeneo mbalimbali ya kuvinjari licha ya kuwepo malalamiko ya kupanda kwa gharama ya maisha.
Baadhi waliozungumza na VOA wanasema hawakuweza kusafiri kwenda vijijini kutokana na kupanda kwa nauli.
Millicent Anyango mkazi wa Nairobi anasema alilazimika kusherekea siku hii muhimu katika kalenda ya wakristo mbali na familia yake kutokana na ugumu wa maisha.
“Nilitamani sana kusafiri ila nisingeweza, nauli imeongezeka maradufu, nikaona bora niwatumie wazazi wangu fedha hizo nao washerehekee japo ningependa kusherehekea nao kama ilivyo desturi yetu”.
Forum