Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 12:39

Wataalam, wanasiasa wamkosoa Trump kuiondoa Marekani WHO


Rais Donald Trump na Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom wakiwa Ujerumani wakati wa mkutano wa G20, 2017.(Photo by SAUL LOEB / AFP)
Rais Donald Trump na Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom wakiwa Ujerumani wakati wa mkutano wa G20, 2017.(Photo by SAUL LOEB / AFP)

Wanasiasa wengi na watalamu wa Marekani wamekosoa uamuzi wa Rais Donald Trump kuiondoa Marekani kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Baada ya miaka 70 ya uwanachama, Marekani inajiondoa kutoka WHO wakati wa mvutano na China juu ya janga la virusi vya corona. China imekosoa uamuzi huo wa Washington.

Mwenyekiti wa kamati katika baraza la Seneti Marekani, Lamar Alexander alitoa taarifa akipinga uamuzi wa Trump akisema hatua hiyo itaingilia kati majaribio ya maabara ambayo ni muhimu katika utengenezaji wa chanjo.

Seneta Mdemokrat katika kamati ya masuala ya kigeni, Bob Mendez alisema Jumanne kupitia ujumbe wa Twitter kwamba Rais Trump aliliarifu rasmi bunge kwamba Marekani imechukua hatua rasmi ya kujiondoa kutoka Shirika la Afya duniani WHO.

Katika ujumbe wake amesema jambo hilo linawaacha Wamarekani wakiwa wagonjwa na Marekani kuwa katika hali ya upweke.

Mgombea kiti cha rais wa chama cha Democratic, Joe Biden anayetarajiwa kupambana na rais Trump hapo Novemba ameandika ujumbe kwamba akichaguliwa Marekani itarudi tena kwenye WHO.

Eric Feigl-Ding Mtaalamu wa magonjwa ya milipuko katika chuo Kikuu cha Harvard, anatoa hoja kwamba hatua kama hiyo inabainisha kwamba Marekani haitaki kushirikiana kuhusiana na haki miliki za chanjo za ugonjwa wa COVID-19.

Amesema wanaitaka hati miliki na vile vile wakijiunga na WHO, basi makampuni yanayojiunga yatabidi kutoa sehemu za hati miliki na makampuni ya Marekani hayataki kufanya hivyo. Na Marekani inataka kumiliki chanjo hiyo kwanza.

Rais Trump ameikosoa WHO kwa kuipendelea China kuhusiana na janga la COVID-19, na katika barua yake kwa Mkurugenzi wa WHO Tedros Adhamon Ghebreyesus mapema mwezi Mei, Trump alitishia kusitisha mchango wake kwa WHO ikiwa shirika hilo la imnataifa halitafanya marekebisho katika muda wa siku 30.

China nayo Jumatano imekosoa uamuzi huo ikieleza kwamba hatua hiyo itakuwa na athari mbaya kwa nchi zinazoendelea, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje Zhao Lijian anaisihi jumuia ya kimataifa kuimarisha msaada wao kwa WHO.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China : "Tunatoa wito kwa jumwiya ya kimataifa kuungana zaidi katika utaratibu wa ushirikiano wa kimataifa na kuongeza uwekezaji na uungaji mkono kwa shirika la afya duniani na kulinda usalama wa afya ya umma kimataifa."

Hivi sasa itachukua mwaka mmoja kabla ya Marekani kujiondoa kutoka shirika hilo lenye makao yake Geneva na kulipa madeni yake yote. Kulingana na mtandao wa WHO Marekani inadaiwa zaidi ya dola milioni 200 ya michango yake.

XS
SM
MD
LG