Kwa mara ya pili mwaka huu, Marekani imelisafirisha kundi la Wasomali kwenda nchini kwao.
Wale waliorejeshwa Somalia walifuatana na mwakilishi wa Uhamiaji na Forodha wa serikali ya Marekani, aliye wakabidhi wahamiaji hao kwa vyombo vya usalama vya Somalia, maafisa wamesema.
Mmoja kati ya wale waliorejeshwa ni Nur Mohamed Mohamud, ambae ameiambia VOA kuwa alisafiri kupitia zaidi ya nchi kumi kwa kipindi cha miezi miwili mpaka kufika Marekani.
Amesema alikuwa amewekwa kizuizini Florida kwa miezi 20 kabla ya kurejeshwa Somalia. “Walinikatalia ombi langu la ukimbizi. Mimi sikuwa mhalifu,” amesema.
Mohamud amesema ubalozi wa Somalia Washington ulitoa hati za kusafiria za wanaorejeshwa zilizowezesha zoezi hilo kufanyika.
Kaimu Waziri wa Usalama wa Ndani wa Somalia Abdirizak Omar Mohamed ameviambia vyombo vya habari vya taifa kwamba serikali ilipewa taarifa kuhusu kurejeshwa kwa watu hao kabla hawajawasili Mogadishu.
“Hakuna mkataba kati ya serikali ya Somalia na Marekani kuhusu wahamiaji, lakini wahamiaji hawa waliorejeshwa ni raia wa Somalia ambao walikuwa na matatizo na walikuwa kizuizini na wao ndio waliomba kurejeshwa Somalia,” amesema.
Hii ni mara ya pili Marekani imewaondoa wahamiaji wa Somalia tangia Donald Trump alipokuwa rais wa Marekani Januari 20. Kundi la kwanza la Wasomali 90 walirejeshwa kwa ndege Somalia mwisho wa mwezi wa Januari.
Balozi wa Somalia nchini Marekani, Ahmed Isse Awad, ameiambia VOA wakati wahamiaji hawa walipotuma barua ubalozini Washington wakiomba kusafirishwa, wote hawa walikuwa kizuizini au jela.
Somalia ni moja ya nchi sita ambazo zimeathiriwa na amri mpya iliyofanyiwa marekebisho ya kusafiri iliyotolewa na Trump.
Rais wa Somalia Mohamed Abdullahi Farmajo amemwomba Trump kuondosha pingamizi la kusafiri kwa wananchi wa Somalia wanaotaka kuja Marekani.