Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 09:17

Jamii ya Washona washerehekea hadhi ya uraia nchini Kenya


Jamii ya Washona nchini Kenya wamekuwa hawana utaifa kwa zaidi ya miaka 50. (photo courtesy: Chief Joshua Kimemia)
Jamii ya Washona nchini Kenya wamekuwa hawana utaifa kwa zaidi ya miaka 50. (photo courtesy: Chief Joshua Kimemia)

Msukumo wa kuwatambua kama Wakenya uliongezeka zaidi ya miaka minne iliyopita

Watu wa jamii ya Washona nchini Kenya wanasherehekea hadhi yao mpya kama raia wa nchi hiyo baada ya miongo kadhaa ya kutokuwa na nchi.

Nazizi Dube anatazama kile ambacho sasa ni milki yake yenye thamani kubwa kwake hati inayomtangaza kuwa raia wa Kenya.

Dube ni mmoja kati ya Washona karibu 1,700 na Wanyarwanda 1,300, ambao walipata hadhi hiyo ya kisheria mwezi huu baada ya miongo kadhaa ya kutokuwa na nchi.

Desemba 12, wakati Kenya ilipoadhimisha miaka yake 57 ya uhuru, Nazizi, na wengine wa jamii ya Washona nchini Kenya walitambuliwa kama raia, kufuatia agizo la Rais Uhuru Kenyatta wa nchi hiyo.

“Changamoto zote ambazo tumepitia na hali ya kutokuwa na utaifa, tulifurahi sana kujua kwamba yote haya yameisha, ulikuwa mwanzo mpya.” Alisema Nazizi Dube.

Mwanzo ambao wanatumai utafungua fursa mpya. Diana Gichengo, wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, anasema kwamba miongo kadhaa ya kutokuwa na utaifa iliiacha jamii hiyo ikitengwa

“Walipokuwa hawana utaifa haki zao zote zilikiukwa, uhuru wao wa kutembea ulikiukwa, wasingeweza kuondoka nchini, wale wachache waliofanikiwa kusafiri walilazimika kupata vitambulisho bandia au visivyo vya kawaida kusafiri, hawakuweza kupata elimu.” Alisema Gichengo.


Ishmael Dlamini ameendesha biashara yake ya useremala nje kidogo ya mji mkuu Nairobi kwa karibu miaka 20 bila hati za kitambulisho. Kama Mshona, mapato yake yalikuwa machache kwa sababu hakuweza kuyapitisha benki au kukopa, kama raia wa Kenya wanavyofanya. Hilo limebadilika.
Dlamini anasema, “tutakuwa na cheti cha uraia. Anasema itaniwezesha kwenda benki au taasisi nyingine yoyote ya kukopesha na kupata mkopo kuniruhusu kufanya biashara zaidi.”

Washona walianza kuwasili Kenya katika miaka ya 1930, kutoka Zimbabwe, na wengi zaidi walikuja mwanzoni mwa miaka ya 1960 wakiwa wamishonari. Lakini wakati Kenya ilipopata uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1963, wengi walishindwa kutumia fursa ya muda wa miaka miwili kuwa raia, pamoja na watoto wao waliozaliwa nchini humo.

Msukumo wa kuwatambua kama Wakenya uliongezeka zaidi ya miaka minne iliyopita.

Wanja Munaita wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Wakimbizi, amepokea vyema uamuzi wa kuwapatia uraia wa washona.

"Utambulisho wa kisheria ni muhimu sana haswa kwa kuwa Kenya inaingia kwenye vitambulisho vya dijitali kwa sababu wangeachwa nje ya mfumo huo, kwa sababu hawakuwa na hati hizo.” Alisema Munaita

Gichengo wa Tume ya Haki za Binadamu ya Kenya, ambayo ilihusika katika kampeni ya kukomesha ukosefu wa utaifa, anasema mengi zaidi yanahitaji kufanywa ili kusaidia jamii ya Washona.

“Tunatumai kuwa wanaweza kuungwa mkono na serikali ya kitaifa na serikali ya kaunti kwa suala la hatua ya kuthibitisha, kuendana na miaka ambayo wametengwa.” Alisema Gichengo.

Inakadiriwa washona 1,300 bado hawajaomba uraia lakini, wale wanaosubiri vtetu vyao wanasema wako tayari kudhibitisha.

“Tunataka kuonyesha kuwa sisi sio tu mzigo kwa nchi sisi ni ndege wenye manyoya yanayong’aa. Hatustahili kufungiwa kwenye tundu. Sasa tunataka kuruka na kuonyesha manyoya yetu angavu.” Alisema Dube.

Shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa linasema Kenya ni nyumbani kwa watu wapatao 18,000 wasio na utaifa, wengi wao wakiwa makabila madogo.

Imetayarishwa na Sunday Shomari, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG