Washauri wa usalama wa kitaifa wa zamani wa chama cha Republikana, pamoja na wakuu wa ujasusi na wawakilishi wa biashara wametia saini barua isemayo kwamba hakuna hata mmoja wao atampigia kura mgombea kiti cha rais wa marekani Donald Trump.
Maafisa hao wa zamani wamemtumikia kila rais Mrepublikan, kuanzia Richard Nixon hadi George W Bush, na ni pamoja na mkuu wa zamani wa CIA, Michael Hayden, wakurugenzi wa zamani wa usalama wa ndani, Michael Chertoff na Tom Ridge. Wengine ni pamoja na mwakilishi wa zamani wa kibiashara, Carla Hills, na baadhi ya waliokuwa manaibu wa Mawaziri katika serikali ya Marekani.
Barua hiyo imesema kuwa sio tu kwamba Donald Trump hafai kuwa rais wa Marekani, lakini kwamba atakuwa rais hatari sana kwa Marekani.