Wapiganaji wa kundi la M23 mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wanaendelea na mashambulizi yao kama walivyo ahidi kwa kuteka miji zaidi siku ya Ijuma.
Mapigano makali yaliripotiwa katika mji wa Sake magharibi ya Goma mji mkuu wa Kivu Kaskazini, na kufikia Alhamisi usiku wakuu wa M23 walidai kwamba wamewarudisha nyuma majeshi ya serikali yaliyojaribu kuwaondowa kutoka ngome hiyo yao.
Ijuma asubuhi wapiganaji waliripotiwa kuingia katika mji mwngine wa Minova wakielekea kusini katika lengo la kuingia Kivu Kusini.
Wakati mapigano yalipokuwa yanandelea Rais Joseph Kabila alimsimamisha kazi mkuu wa jeshi la nchi kavu Jenerali Gabriel Amisi, akituhumiwa kwenye ripoti moja ya Umoja wa Mataifa, kwamba amekuwa akiendesha mtandao wa kusambaza silaha kwa wawindaji haramu na makundi ya waasi, likiwemo kundi la Mai Mai Raia Mutomboki.
Jenerali Amisi amekanusha ripoti hizo. Msemaji wa serikali Labert Membe amesema mkuu huyo amesimamisha kazi wakati uchunguzi unaendelea.
Mazungumzo ya Amani Kampala
Katika juhudi za kutafuta suluhisho kwa mzozo huo wa mashariki ya Congo Rais Yoweri Museveni aliwapelekea viongozi wa M23 helikopta na kuwasafirisha hadi Kampala ambako tayari Marais Paul Kagame na Joseph Kabila wanakutana kulijadili suala hilo la uwasi wa mashariki ya Congo.
Siku ya Jumamosi viongozi 11 wa mataifa ya kanda ya Maziwa Makuu wanakutana pia Kampala kujadili juu ya kupelekwa kikosi cha Kiafrika kupambana na makundi ya waasi huko mashariki ya Kongo.
Msemaji wa M23 aliambia Sauti ya Amerika kwamba walivamia Goma katika lengo la kumlazimisha Rais Kabila kuzungumza nao juu ya madai yao.
Tanzania na Burundi za onya kwamba uvamizi wa M23 huko Goma kutazusha matatizo makubwa kwa nchi za kanda hasa watu wanaokimbia vita. Mawaziri wa mambo ya nchi za nje wa Tanzania na Burundi wamewataka waasi hao kuondoka Goma mara moja