Wapalestina wameanza kuwasili huko Gaza City mapema Jumatatu, wakati vikosi vya Israel vilipofungua vituo vya ukaguzi na kuwaruhusu watu kurejea katika maeneo ya kaskazini ambayo yalikuwa yamefungwa tangu siku za mwanzo za vita vya Israel dhidi ya Hamas.
Maelfu ya watu wengi wao wakitembea kwa miguu, walikuwa barabarani kuelekea Gaza City ambayo imeshuhudia uharibifu mkubwa wakati wa operesheni za ardhini za Israel na mashambulizi ya anga ambayo jeshi lilisema yalilenga kuliangamiza kundi hilo la wanamgambo.
Gaza City ni moja ya maeneo mengi ambayo yalikabiliwa na amri ya Israel ikiwataka waondoke, na kuwaacha watu wakihangaika kutafuta mahali salama wakati wa vita. Wengi wa wahamaji walihamishwa mara kadhaa na kurejea kwenye kambi za mahema kwa ajili ya makazi.
Kurejea kwa Wapalestina huko Gaza City kunatokea kufuatia makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hamas ambayo pia yamejumuisha kuachiliwa kwa baadhi ya mateka wanaoshikiliwa huko Gaza, kuwaachia huru wafungwa wa Kipalestina wanaoshikiliwa na Israel, na kuongezeka kwa misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.
Forum