Katika michuano ya Olympiki ya riadha inayoendelea huko Tokyo Japan, mwanariadha wa Ivory Coast Marie-Josee Ta Lou aliweka rekodi mpya ya Afrika kwa wanawake katika mbio za mita 100 wakati aliposhinda katika raundi ya awali kwa sekunde 10.78 na kufanikiwa kusonga mbele kwenye nusu fainali ya michuano hiyo Ijumaa.
Katika raundi ya tatu ya michuano hiyo Ta Lou alichukua uongozi katikati ya mbio hizo na kuweka moja ya rekodi ya juu ya kasi kuwahi kutokea katika raundi ya kwanza ya mita 100 za Olimpiki.
Wanariadha wengine wa Afrika ambao walifuzu kuingia nusu fainali ni pamoja na wanigeria Blessing Okagbare ambaye alishinda raundi ya awali kwa sekunde 11.05 na Grace Nzubechi Nwokocha ambaye aliweka rekodi nzuri ya sekunde 11. Murielle Ahoure wa Ivory Coast pia alifuzu kuingia nusu fainali baada ya kumaliza akiwa nambari tatu akitumia sekunde 11.16. Gina Bass wa Gambia aliweka rekodi mpya ya kitaifa ya sekunde 11.12 na anaweza kufuzu kuingia nusu fainali kulingana na muda wa kasi zaidi.
Na katika michuano ya kikapu timu ya Wanawake ya Nigeria D Tigers iliangushwa na Ufaransa kwa jumla ya pointi 69-86.