Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 03:39

Wanamgambo wazidiwa nguvu Msumbiji


Wanajeshi wa Msumbiji washika doria kwenye mji wa Mocimboa da Praia
Wanajeshi wa Msumbiji washika doria kwenye mji wa Mocimboa da Praia

Ripoti iliyotolewa Jumapili inasema kuwa vikosi vya Rwanda na Msumbiji vimechukua tena udhibiti wa mji wa bandari wa Mocimboa da Praia nchini Msumbiji, ukiongezwa kwenye orodha ya miji ambayo imekombolewa hivi karibuni kutoka kwenye mikono ya wanamgambo wa kiislamu.

Jimbo la kaskazini mwa Msumbiji la Cabo Delgado lenye utajiri mkubwa wa gesi inayosemekena kuwa na thamani ya takriban dola bilioni 60 limekuwa likivamiwa na wanamgambo wa kiislamu tangu mwaka 2017. Kuanzia mwaka uliopita, wanamgambo hao wameongeza mashambulizi wakati wakichukua udhibiti wa miji muhimu ukiwemo ule wa bandari wa Mocimboa da Praia.

Mwezi uliopita, serikali ya Rwanda ilituma wanajeshi 1,000 nchini Msumbiji ili kusaidiana na vikosi vya Msumbiji, pamoja na vile kutoka mataifa 16 wanachama wa SADC, kukabiliana na wanamgambo hao. Mji wa Mocimboa da Praia uko kilomita 60 kusini mwa eneo lenye miradi ya gesi, wakati bandari yake ikutumika kupokea bidhaa kutoka mataifa ya nje.

Msemaji wa kikosi cha Rwanda nchini humo Ronald Rwivanga ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wanamgambo hao walilazimika kukimbilia kwenye misitu iliyoko karibu baada ya kuupoteza mji huo ambao wameushikilia tangu mwaka uliopita. Rwivanga ameongeza kusema kuwa hilo ni pigo kubwa sana kwa wanamgambo hao na kwamba wanajeshi wataendelea kuulinda mji huo hadi hali ya kawaida irejee.

Kanali Omar Saranga, msemaji wa wizara ya ulinzi ya Msumbiji amewaambia wanahabari Jumapili kwamba vikosi vilichukua tena udhibiti wa maeneo binafsi pamoja na ya umma yakiwemo majengo ya serikali, hospitali, masoko na migahawa. Ripoti zinaongeza kusema kuwa vikosi hivyo pia vimechukua udhibiti wa mji mdogo wa Awasse ulioko karibu na Mocimboa da Praia.

Mtayarishaji - Harrison Kamau

XS
SM
MD
LG