Waziri wa ulinzi wa Uingereza Ben Wallace hata hivyo amesema kwamba Russia bado ni tishio katika sehemu hiyo.
Amesema kwamba hatua ya wanajeshi hao kuondoka Kherson ni ishara za kufeli kimkakati.
Wanajeshi wa Russia wameziachilia sehemu tatu muhimu kufikia sasa, ambazo wamekuwa wakizidhibiti, kutokana na mashambulizi makali kutoka kwa jeshi la Ukraine. Kherson ndio mji mkubwa zaidi kuachiliwa na wanajeshi hao.
Wallace amesema kwamba jeshi la Russia limepata hasara kubwa sana na kwamba Ukraine itaendelea kupata msaada kutoka Uingereza na jumuiya ya kimataifa.
Hata hivyo, ameonya kwamba Russia bado ni tishio kubwa kwa Ukraine katika vita hivyo.
Uturuki ina nia ya dhati kumaliza vita Ukraine - Erdogan
Wakati huo huo, Uturuki imesema kwamba ina nia ya dhati kuhakikisha kwamba majadiliano ya amani kati ya Russia na Ukraine yanafanikiwa.
Vyombo vya habari vya Uturuki vimesema kwamba rais wa Uturuki Recepp Tayip Erdogan amesema hayo huku akiishutumu Marekani na mataifa mengine ya Magharibi kwa kile alichokitaja kama kuichokoza Russia.
Shirika la habari la serikali ya Uturuki TRT, limemnukuu Erdogan akisema kwamba mataifa ya Magharibi hasa Marekani yanaishambulia Russia bila kukoma.
Erdogan hata hivyo hajatoa ufafanuzi zaidi kuhusu matamshi yake.
Amewaambia waandishi wa habari nchini Uzbekistan kwamba Russia inajaribu kujizuia kwa kila njia.
Mataifa ya Magharibi yameipaUkraine silaha ili kuendelea kupigana na Russia.
Mataifa hayo vile vile yamewekea Russia vikwazo kadhaa vya kiuchumi tangu nchi hiyo ilipoivamia Ukraine kijeshi, Febrauri mwaka huu.
Uturuki, ambayo ni mwanachama wa NATO, iliongoza mazungumzo kati ya Ukraine na Russia yaliyopelekea kuanza tena kwa usafirishaji wa nafaka kutoka Ukraine hadi kwenye masoko ya kimataifa.