Marekani imetangaza rasmi kwamba itawarejesha nyumbani wanajeshi wake kadhaa katika siku chache zijazo, kufuatia amri ya rais Donald Trump ya kuondoa karibu wanajeshi 2,000 kutoka Afghanistan na 500 kutoka Iraq kabla ya utawala wa Joe Biden kuingia madarakani.
Kaimu waziri wa ulinzi wa Marekani Chris Miller, amewaambia waandishi wa habari kwamba idadi ya wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan na Iraq itakuwa wanajeshi 2,500 katika kila nchi kufikia Januari 15.
Miller amesema kwamba hatua ya kupunguza wanajeshi hao haitokani na mabadiliko ya sera au malengo ya Marekani kulingana na vita dhidi ya ugaidi na kwamba wanajeshi hao wataondolewa kwa njia itakayohakikisha kwamba wanajeshi wa Marekani wanalindwa, saw ana wanadiplomasia, maafisa wa ujasusi na washirika wa Marekani.
Miller amesema kwamba amezungumza na vionozi kadhaa na kuwaarifu kuhusu mpango huo wa Marekani, wakiwemo viongozi wa bunge, katibu mkuu wa NATO na rais wa Afghanistan Ashraf Ghani.
Muungano wa NATO sasa una wanajeshi wengi zaidi nchini Afghanistan kuliko Marekani na maafisa wa kijeshi wanasema kwamba Pentagon inawasihi kuendelea kuwa na idadi hiyo ya wanajeshi nchini humo hata wakati rais Trump anapunguza idadi ya wanajeshi wa Marekani.